Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 05/07/2024

2024 JULAI 5: IJUMAA; JUMA  LA 13 LA MWAKA

Mt. Elisabeti, Malkia
Rangi: Kijani

Zaburi:

Somo 1. Amo 8:4-6, 9-12

Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini ay eye, mkisema, Mwezi mpya utaondoka lini, tupate kuuza nafaka? Na sabato nayo, tupate kuandika ngano? Mkiipunguza efa na kuiongeza ay ey, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu, tupate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano. Tena itakuwa siku hiyo, asema Bwana Mungu, nitalifanya jua litue wakati wa adhuhuri, ay  nitaitia nchi giza wakati wa nuru wa mchana. Nami nitazigeuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, na nyimbo zenu zote kuwa vilio; ay  nitatia nguo za magunia katika viuno vyote, na upaa katika kila kichwa; ay  nitayafanya haya kuwa kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu. Angalia, siku zinakuja, asema Bwana Mungu, ambazo nitaleta njaa katika nchi, si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana. Nao watatangatanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazini hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione.

Wimbo wa Katikati. Zab 119:2, 10, 20, 30, 40, 131

1. Heri wazitiio shuhuda zake,
wamtafutao kwa moyo wote.
Kwa moyo wangu wote nimekutafuta,
Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.

(K)” Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. “

2. Roho yangu imepondeka kwa kutamani,
Hukumu zako kila wakati.
Nimeichagua njia ya uaminifu,
Na kuziweka hukumu zako mbele yako. (K)

3. Tazama, nimeyatamani mausia yako,
Unihuishe kwa haki yako.
Nalifungua kinywa changu nikatweta,
Maana naliyatamani maagizo yako. (K)

Injili. Mt 9:9-13

Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata. Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.

TAFAKARI

MUNGU WETU NI WA HURUMA: Mungu wetu si mwepesi wa hasira ni mwingi wa huruma (rej. Zab 148:8). Yesu alimwita Mathayo mtoza ushuru. Makundi mengine kama mafarisayo waliwatazama watoza ushuru katika jamii ya wakati huo kama wadhambi. Mafarisayo wenyewe wanaonekana kuwa ni wanafiki wakihesabu bila kuhesabu ya kwao. Yesu alimwona Mathayo akitafuta maana ya maisha, alipomwita, Nifuate, aliacha vyote akamfuata. Maneno ya Kristo yalikuwa ya maana sana kwake alifurahishwa nayo. Tofauti na mafarisayo waliobakia kulaumu na kuwanyooshea kidole wengine. Tunaona pia nabii Amosi anaendelea kuwaalika Waisraeli kuupokea ujumbe wa huruma ya Mungu ulioletwa kwao. Anawatangazia kuwa wasipofanya hivyo watafikwa na mambo makubwa mchana utageuka usiku na mbaya zaidi Neno la Mungu litapotea kabisa kwao. Hayo wanayopewa Waisraeli yanaletwa kwetu ili tupate nafasi ya kujitathmini; ni maonyo tunayopewa pia sisi tusipoutambua ujumbe wa neno la Mungu, tukaupokee, tukafanya toba na kuiishi huruma yake.

Sala: Ee Bwana neema yako ituwezeshe kutambua huruma yako, kuipokea na kuiishi katika maisha yetu.