Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 02/07/2024
2024 JULAI 2: JUMANNE; JUMA LA 13 LA MWAKA
Mt. Eugenia Joubert
Rangi: Kijani
Zaburi:
Somo 1. Amo 3: 1-8; 4: 11-12.
Lisikieni neno hili alilolisema Bwana juu yenu, enyi wana wa Israeli, juu ya jamaa yote niliowapandisha kutoka nchi ya Misri, nikisema,”Ni ninyi tu niliowajua katika jamaa zote zilizo duniani; kwa sababu hiyo nitawapatiliza ninyi maovu yenu yote.” Je! watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana? Je! simba atanguruma mwituni, asipokuwa na mawindo? Mwanasimba atalia pangoni mwake, ikiwa hakupata kitu? Je! ndege ataanguka mtegoni juu ya nchi, mahali asipotegewa tanzi? Mtego utafyatuka juu ya nchi, bila kunasa kitu cho chote? Je! tarumbeta itapigwa mjini, watu wasiogope? Mji utapatikana na hali mbaya, asiyoileta Bwana? Hakika Bwana Mungu hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake. Simba amekwisha kunguruma, ni nani asiyeogopa? Bwana Mungu amenena, ni nani awezaye neno ila kutabiri?” Baadhi yenu nimewaangamiza, kama hapo Mungu alipoiangamiza Sodoma na Gomora, nanyi mkawa kama kinga kilichonyakuliwa motoni; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.”Basi nitakutenda hivi, Ee Israeli; na kwa sababu nitakutenda hivi, ujiweke tayari kuonana na Mungu wako, Ee Israeli.” |
Wimbo wa Katikati. Zab 5: 4b-8
1. Huwi Mungu apendezwaye na ubaya; (K) Bwana uniongoze kwa haki yako. 2. Unawachukia wote watendao ubatili. 3. Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako, |
Injili. Mt 8:23-27
Yesu alipanda chomboni, wanafunzi wake wakamfuata. Kukawa msukosuko mkuu baharini,hata chombo kikafunikizwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema,” Bwana, tuokoe, tunaangamia.” Akawaambia,” Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka,akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu. Wale watu wakamaka wakisema,” Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?” |
TAFAKARI
TUMKIMBILIE KRISTO ANAWEZA YOTE: Watu wanawaogopa simba, wangurumapo wanaona kuna dhoruba wanakimbizana, wanashindwa kufanya toba kwa mwito wa nabii Amosi. Pamoja na kuwa Mungu aliwapenda akawatoa utumwani Misri awalete kwenye nchi ya ahadi. Katika Injili leo wanafunzi wakifuatana na Kristo wakiwa kwenye chombo majini, mawimbi makali yanakipiga chombo, wanafunzi wale wanakimbilia kumwamsha Kristo ambaye alikuwa amechoka na kupumzika. Hawakujua atafanya nini lakini walimkimbilia Yesu, ambaye anayatuliza yale mawimbi kunakuwa na utulivu. Siku hizi za leo kumekuwa na wimbi la watu wanaotumia majina makubwa kama nabii, mfalme, au nabii na mfalme, mchungaji na wengine kujitambulisha kuwa waweza kufanya makubwa, wanasahau kumpa nafasi anayewawezesha, Kristo ambaye ndiye pekee aliye Mchungaji mwema, Mfalme wa wafalme. Kwa kutambua hivyo wale wanafunzi walimwendea walipokutana na dhoroba. Ni mwaliko kwetu sote tusiyumbishwe na hao bali tumkimbilie Kristo katika sala na maombi. |
Sala: Ee Bwana neema yako ituwezeshe kutambua uweza wako na kukumbilia siku zote.