Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 30/06/2024

2024 JUNI 30: DOMINIKA YA 13 YA MWAKA

Rangi: Kijani
Zaburi: 

Somo 1. Hek 1: 13-15; 2:23-24

Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea. Kwa maana aliviumba vitu vyote ili vipate kuwako, na nguvu za uzazi zilizomo ulimwenguni ni za kuleta siha, wala hakuna ndani yake sumu yo yote ya uharibifu, wala ahera haina milki kama ya kifalme hapa duniani; Maana haki yaishi milele. Yaani, Mungu alimwumba mwanadamu ili apate kutokuharibika, kwa mfano wake mwenyewe, ila ulimwengu uliingiwa na mauti kwa husuda yake Shetani, nao walio wa upande wake hupata kuionja.

Wimbo wa Katikati. Zab 30: 2-6, 11-13

1. Bwana nitakutukuza kwa maana umeniinua,
Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
Umeniinua nafsi yangu,
Ee Bwana kutoka kuzimu.
Umeniuhisha na kunitoa
Miongoni mwao washukao shimoni.

(K) Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua.

2. Mwimbieni Bwana Zaburi,
Enyi watauwa wake.
Na kufanya shukrani.
Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.
Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,
Katika radhi yake mna uhai.
Huenda kuliko huja kukaa usiku,
Lakini asubuhi huwa furaha. (K)

3. Ee Bwana, usikie, unirehemu,
Bwana uwe msaidizi wangu.
Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;
Ee Bwana, Mungu wangu,
Nitakushukuru milele. (K)

Somo 2. 2 Kor 8: 7, 9, 13-15

Kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote; na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake. Maana sisemi hayo, ili wengine wapate raha nanyi mpate dhiki; bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe sawasawa. Kama ilivyoandikwa, aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa. 

Injili. Mk 5: 21-43

Yesu alipokwisha kuvuka kurudi ng’ambo katika kile chombo, wakamkusanyikia mkutano mkuu; naye alikuwa kando ya bahari. Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi. Akaenda pamoja naye. Mkutano mkuu wakamfuata, wakimsongasonga. Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya; aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule. Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, Je! wawaona makutano wanavyokusonga-songa, nawe wasema, Ni nani aliyenigusa? Akatazama pande zote ili amwone yule aliyelitenda neno hilo. Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote. Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena. Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu. Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro, na Yakobo, na Yohane nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula.  

TAFAKARI.

IMANI HUPONYA
Mwenyezi Mungu ameuumba ulimwengu katika ukamilifu wake na kwa namna ya pekee amempatia mwanadamu cheo kikubwa kuliko viumbe vyote kwa kumfanya kwa mfano wa sura yake (rej Mwa 1:26ff). Mzaburi anajiuliza juu ya upendeleo aliopewa na Mungu akisema: “Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako… mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; umemvika taji ya utukufu na heshima” (Zab 8:3 – 4). Hivyo tangu mwanzo mwanadamu hakuumbwa katika uovu au ukosefu wa namna fulani. Ameumbwa katika ukamilifu wote na kupewa utukufu na heshima ya kipekee. Mwanadamu ameinuliwa sana na kupewa hadhi ya kutawala na kuratibu kazi yote ya uumbaji. Katika ukweli huu tunapatwa na mkanganyiko pale tunapoona mambo mabaya yamemwelemea mwanadamu.
Je, mambo haya mabaya yametokea wapi? Je, chanzo chake kinaweza kuwa ni Mungu? Wanafalsafa na wanatauhidi wa kimaadili wanaelezea jambo lolote baya kama ukosefu wa ukamilifu. Kwa maneno mengine ni ukosefu wa uhalisia wa kitu. Hivyo mambo mabaya husababisha upungufu na matokeo yake ni utendaji hafifu au kukosekana kwa utendaji uliokusudiwa. Ubaya ni hitilafu inayoingia katika mfumo au mtindo fulani wa maisha. Kiroho ubaya huonekana kama uovu na unaelezewa kwa neno “dhambi”. Hii ni namna ambayo inamkuta mwanadamu anapokosa utii kwa amri na maagizo ya Mungu, matokeo ya uasi kwa Mungu. Mwanadamu aliyeumbwa kikamilifu kiroho, kimwili na kiakili anaingia katika uovu pale anapokosa hali fulani ya ukamilifu kadiri ya uumbaji na matokeo yake huwa ni ugonjwa, mahangaiko, mifadhaiko ama kuingia katika hali ya mauti kimwili au kiroho.
Masomo ya Dominika ya leo yanatutafakarisha juu ya chanzo cha uovu ambao ni huzuni kwa mwanadamu na mwarobaini wake unakuja kwa njia ya Yesu Kristo. Somo la kwanza linatuonesha chanzo cha uovu. Mauti si mpango wa Mungu bali imemuingia mwanadamu sababu ya wivu wa ibilisi. Mwandishi wa kitabu cha Hekima anaweka wazi kabisa kwamba Mungu amemuumba mwanadamu kwa maisha ya umilele na kutokuharibika, yaani kushiriki pamoja na Mungu katika heri ya milele. Yeye ameviumba vitu vyote vizuri (rej. Mwa 1:31). Mwanadamu ameumbwa katika utakatifu. Tangu uumbaji mwanadamu amekirimiwa tunu hii ya kimungu. Hivyo kubaki mwaminifu kwa Mungu ndiyo ilikuwa kibali kwake katika kuutunza utakatifu wake.
Kifo kinacholetwa na dhambi si kifo cha kimwili bali ni ule utengano kati ya mwanadamu na Mungu sababu ya hukumu ya dhambi. Kwa maneno mengine, mwanadamu anapokuwa bila Mungu anakuwa katika hali ya ukosefu na kupungukiwa. Dhambi ya asili inalifafanua wazi jambo hili. Mwanadamu alikengeuka na kutaka kutenda mambo bila Mungu ili kujitwalia nafasi ya Mungu katika maisha yake. Ni hali ambayo inaendelea kuonekana hata leo katika jamii ya kisekulari amabayo inafanya bidii ya kuigawa dini na maisha ya kawaida ya mwanadamu. Matokeo yake yanashuhudiwa kila uchwao kwa anguko kubwa la mwanadamu. Vita, magonjwa, malumbano, unyonyaji na mengineyo mengi na matunda ya juhudi hizo za kiutu za kumwondoa mwenyezi Mungu na katika maisha ya kila siku. Uovu unaomtafuna mwanadamu unaletwa na mwanadamu mwenyewe.
Injili inatuwekea mbele yetu Kristo kama mwarobaini wa msiba huu mkubwa unaomwandama mwanadamu. Matukio mawili ya uponyaji na uuhishaji ambayo yanarudisha furaha katika jamii ya mwanadamu yanatawaliwa na dhana ya imani. Imani thabiti kwa utendaji wa Mungu ndiyo uliomsukuma aliyeteseka kwa muda mrefu kujongea kwa Kristo kwa ujasiri, bila kujali umati wa watu au hali yake au namna alivyopokeleka sababu ya hali yake na matokeo yake anapona msiba wake: “Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule.” Hali kadhalika kwa mkuu wa sinagogi; bila kujali nafasi yake katika jamii katika masuala ya kidini anaitambua nguvu ya Mungu inayotenda ndani ya Kristo na kwa imani anaomba uponyaji kwa binti yake.
Kristo alimwambia yule mama, “Imani yako imekuponya.” Kwa upande wa mkuu wa sinagogi alimwambia, “usiogope, amini tu.” Imani inarudisha urafiki kati ya mwanadamu na Mungu. Imani inamfanya mwanadamu atambue kuwa bila Mungu hawezi kufanya kitu chochote kwa ukamilifu; anapojitenga na Mungu anakuwa na masuluhisho ya muda mfupi. Huo ndio mwarobaini anaotuletea Kristo katika jamii yetu leo hii. Pamoja na zawadi hii bado tunatahadharishwa uwepo wa ukinzani kutoka kwa watu ambao wanatuzunguka. Wapo ambao kama mitume pamoja na kuwa karibu na Kristo wanashindwa kuona nguvu ya Kristo na kutaka jambo hilo lipite tu; wapo ambao kama wale ndugu kule nyumbani wanatucheka na kutudhiaki na pengine kutuona kama wendawazimu lakini Kristo anaendelea kutuambia: “usiogope, amini tu.”
Injili ya leo inatuonesha namna mbili zinazotufikisha katika kuionja nguvu ya Mungu ya uponyaji kwa njia ya imani. Kwanza ni kwa njia ya kupelekwa na na watu wengine. Hapa tunakumbushwa wajibu wetu wa kuombeana na kushirikishana utajiri wa kiroho kusudi kuufikia ukombozi tunaopewa kwa njia ya Kristo. Hii ni namna ambavyo tunaguswa na mahangaiko ya watu wengine na hivyo tunakuwa wajumbe wa kuufunua uso wa huruma ya Mungu kwao kwa sala zetu na maisha yetu ya ushuhuda. Pili ni pale tunapojongea sisi wenyewe kuiendea huruma ya Mungu. Baada ya mahubiri, maelekezo na mifano mbalimbali kutoka kwa wapendwa wetu tunavutwa kwenda kwa Kristo. Namna hii ya pili inaonekana katika namna njema ya kugusa bila kujulikana lakini Yeye aonaye sirini atakuinua mwenyewe. Hapa inaonekana dhana ya unyenyekevu na subira katika kuujongea uponyaji wa Mungu. Namna zote hizo mbili zinachagizwa na paji la imani. Haya yote yanatudai unyenyekevu, subira na upole.
Wajibu wetu kama Wakristo unafafanuliwa zaidi na Mtume Paulo anapowaasa Wakristo wa Korinto juu ya umuhimu wa kutajirishana wao kwa wao ili mwishoni kusiwepo na aliyezidi au aliyepungua huku akimweka Kristo kama mfano: “aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala aliyekusanya vichache hakupungua.” Upendo huu wa kushibishana ni tunda la imani thabiti kwa Mungu. Mwanadamu atakapomweka mwenyezi Mungu kuwa sababu na chanzo cha yote aliyonayo upendo wake kwa Mungu utakua na hivyo ataiona sura ya Mungu katika nafsi ya ndugu yake. Kujifungua kiroho kwa wenzetu na kuwa tayari kuwaangazia wengine nguvu na uwezo wa Mungu na kwa njia hiyo tunaimarisha undugu kati yetu sisi kwa sisi na kujenga umoja madhubuti na Mungu muumba wetu. Mama yetu Bikira Maria, aliyechagizwa na imani thabiti kwa Mungu hata kuwa tayari kuitikia ‘ndiyo’ kwa wito wake na kutuletea mkombozi, yaani mwanae Yesu Kristo, atuombee.

SALA: Ee Yesu uguse maisha yetu kwa Neno na Sakrementi zako.