Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 29/06/2024

2024 JUNI 29: JUMAMOSI; JUMA  LA 12 LA MWAKA

WAT. PETRO NA PAULO, MITUME
Rangi: Nyekundu

Zaburi: Tazama Sala ya Siku

Somo 1. Mdo 12:1-11

Herode mfalme alinyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohane, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa amelala katikati ya askari wawili amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, “Ondoka upesi.” Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, “Jifunge, Kavae, viatu vyako.” Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, “jivike nguo yako ukanifuate.” Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu akasema, “Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono ya Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi.”

Wimbo wa Katikati. Zab 34:1-8

1.  Nitamhimidi Bwana kila wakati,
     Sifa zake kinywani mwangu daima.
     Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
     Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.

(K) Malaika wa Bwana awaokoa wamchao.

2.  Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
     Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
     Nalimtafuta Bwana akanijibu,
      Akaniponya na hofu zangu zote. (K)

3.  Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
      Wala nyuso zao hazitaona haya.
      Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
      Akamwokoa na taabu zake zote. (K)

4.    Malaika wa Bwana hufanya kituo,
      Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
     Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema,
      Heri mtu yule anayemtumainia. (K)

Somo 2. 2 Tim 4:6-8, 17-18

Mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, Mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba. Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una yeye milele na milele. Amina.

Injili. Mt 16:13-19

Yesu alienda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, “Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” Wakasema, “Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.”  Akawaambia, “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” Simoni Petro akajibu akasema, “Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Yesu akajibu, akamwambia, “Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.”

TAFAKARI

MUNGU ANA MPANGO NA KILA MMOJA WETU: Leo Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Miamba ya Imani ya Kanisa Katoliki: Mtume Petro na Mtume Paulo. Historia ya mitume hawa ni tofauti, japo wanakutana sehemu moja: wote wamemwaga damu yao kwa ajili ya Kristo. Petro, mwenyeji wa Bethsaida mvuvi wa samaki aliyeitwa na Yesu kuwa mvuvi wa watu pale walipoambiwa “Nifuateni, nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu”(Mt 4:18-22). Ndiye Petro huyu aliyeungama U-Mungu wa Yesu pale aliposema “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai”(Mt 16:16). Mtume Paulo kwa upande wake, mwenyeji wa Tarso, alikuwa adui mkubwa wa wafuasi wa Kristo kiasi cha kuwaua. Alipata kuongoka akiwa katika moja ya safari zake za kutesa wakristo huko Dameski. Akiwa njiani alipigwa na mwanga ghafla na sauti ikasikika ikimwambia “Sauli, Sauli! Kwanini unanitesa? “(Mdo 9:3-4). Njia za Mungu si njia za mwanadamu. Mungu humteua yeyote anayemtaka ili afanye kazi yake. Kanisa leo linawashangilia kama mashujaa wa imani, walimu wa imani na waombezi wa Kanisa. 

SALA: Ee Yesu utufanye tuwe vyombo vyako vya uinjilishaji.