Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 23/06/2024

2024 JUNI 23 : DOMINIKA YA 12 LA MWAKA

DOMINIKA YA 12 YA MWAKA
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 

Somo 1. Ayu 38: 1, 8-11

Bwana alimjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, Ni nani aliyeifunga bahari kwa milango, Hapo ilipofurika kana kwamba imetoka tumboni. Nilipolifanya wingu kuwa vazi lake, na giza zito kuwa nguo ya kuifungia, Nikaiagiza amri yangu; Nikaiwekea makomea na milango, Nikasema, Utafika mpaka hapa, lakini hutapita, Na hapa mawimbi yako yanyetayo yatazuiliwa?

Wimbo wa Katikati. Zab 107: 23-24. 25-26. 28-29. 30-31 (1b)

1. Washukao baharini katika merikebu,
Wafanyao kazi yao katika maji mengi,
Hao huziona kazi za Bwana,
Ma maajabu yake vilindini.

(K) “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele”

2. Maana husema, akavumisha upepo wa dhoruba,
Ukayainua juu mavumbi yake.
Wapanda mbinguni, watelemka vilindini,
Nafsi hao yayeyuka kwa hali mbaya. (K)

3. Wakamlilia Bwana katika dhiki zao,
Ajawaponya na shida zao.
Huituliza dhoruba, ikawa shwari,
Mawimbi yake yakanyamaza. (K)

4. Ndipo walipofurahia kwa kuwa yametulia;
Naye huwaleta mpaka bandari waliyoitamani.
Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake,
Na maajabu yake kwa wanadamu (K)

Somo 2. 2 Kor 5: 14-17

Upendo wa Kristo watubidisha; maana tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote; tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao. Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwii, lakini sasa hatumtambui hivi tena. Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo mekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya.

Injili. Mk 4: 35- 41

Siku ile kulipokuwa jioni, Yesu aliwaambia, Na tuvuke mpaka Ng’ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambi, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?
NYAKATI ZA DHORUBA MTAZAME KRISTO
Mwanadamu anapoingia katika changamoto za kimaisha huwa ni mwepesi kutoona nguvu ya Mungu, upendo wa Mungu na mara nyingi imani yake kwa Mungu hutetereka. Ni rahisi hapo kuuliza kama kweli Mungu yupo, ana uwezo na anatupenda kwa nini aruhusu mmoja kuingia katika changamoto hii au ile? Washauri wa kiroho mara nyingi wanakuwa na wakati mgumu wa kuwaelekeza walio katika hali hii kuimarisha uhusiano wao na Mungu. Leo tunakumbushwa kuwa hata katika nyakati za dhoruba daima tumtazame Kristo. Mwenyezi Mungu amethibitisha kuwa “fadhili zake ni za milele” (Zab 107:1).
Katika Somo la kwanza tunakutana na habari ya Ayubu. Ayubu anakumbushwa kwamba asikose kumsadiki Mungu hata katika hali ya mateso. Jibu la Mungu kwa Ayubu ambaye alionekana kuyumba katika imani yake kwa Mungu lilinuia kumkumbusha ukuu wa Mungu na utendaji wake. Ayubu alikumbushwa kuwa Mungu ndiye muumbaji wetu na viumbe vyote pamoja na sisi tu mali yake. Mashaka ya Ayubu yaliendana na fikra za kiyahudi kwa wakati huo kwamba Mungu anawaadhibu waovu na mmoja anapokumbana na dhahama yoyote ya kimaisha ni uthibitisho kwamba maisha yake hayakuwa sawa mbele ya Mungu. Mwelekeo huu wa kimawazo ni rahisi kumuondoa mmoja katika utegemezi kwa Mungu na kutoiona nafasi yake katika maisha.
Mawazo kama haya yanaonekana pia katika nyakati zetu, mwelekeo ambao unatuyumbisha na kudumaza imani yetu. Na matokeo yake tunajikuta mara nyingi tunaingia katika kutumaini nguvu nyingine za nje na kujishikamanisha zaidi na ulimwengu. Lakini hali hii haitupatii suluhisho la kudumu. Tunajikuta tunapata auheni kwa kipindi fulani na hali mbaya hurudia tena na wakati mwingine hugeuka na kuwa mbaya zaidi. Tatizo hapa ni nini? Ni kuusahau ukuu wa Mungu na utendaji wake, ni kusahau fadhili zake, ni kusahau kwamba hata hiyo pumzi inayokupatia uwezo wa kufikiri au kuamua unavyoamua bado ni mali ya Mungu.
Mungu anapozungumza na Ayubu leo katika Somo la kwanza anazungumza na wewe pia. Anakukumbusha ukuu na upana wa uwezo wake, anakuonesha jinsi anavyoielekeza nchi na kazi yote ya uumbaji ikae katika uwiano mzuri. Yote hayo yanathibitisha uwepo wake na uwapo wake wa daima. Mwanadamu anausahau uwepo huu wa Mungu. Ajishughulishi kuwa viumbe vyote ni ukamilifu wa Mungu na Mungu yumo ndani yake. Katika Injili Mitume wanapokumbana na dhoruba kali wanaingia na hofu kwa nguvu za nje, vurugu za kazi yote ya uumbaji na kusahau mara moja kuwa yumo ndani yao Yeye asiyeshindwa na lolote. Badala ya kuinua macho yao na kumwangalia yeye wanaendelea kuangalia na kuymbishwa na upepo wa kidunia.
Yesu anapowaagiza Mitume wake kuchukua chombo na kuvuka ng’ambo ni ishara ya safari yetu ya kiroho ambayo inatuelekeza kufika upande wa pili ambako tutapata uzima wa milele. Safari hii si nyepesi hivyo. Tutakumbana na changamoto nyingi sana za kimaisha. Mawimbi ya maisha ndiyo maovu na upinzani tunaokutana nao katika safari ya imani. Je, tunaitikiaje imani yetu na kuyakabili mawimbi haya? Je, tunauona uwepo wa Yesu katikati yetu? Yeye anakaa na sisi katika Neno lake, kwa njia ya masakramenti na kwa namna ya pekee Ekaristi Takatifu. Hivyo tunaalikwa katika Dominika hii kunoa tena imani yetu, kufungua macho yetu ya ndani ili kuutambua uwepo wa Kristo na kujitegemeza kwake siku zote.
Tunapoangalia jamii yetu leo hii na kutangatanga kwingi kwa watu yapo mengi ya kujiuliza juu ya imani. Je, kama wameshindwa kumuona Kristo na utendaji wake huku alipo ni nini ambacho kitawafanya wamuone huko waendako? Je, huko waendako kuna Kristo wa aina nyingine? Tatizo si kukosekana kwa Kristo bali ni utayari wa mtu binafsi kujifunua na kumwona Yeye aliye ndani yake. Wakati mwingine huwa tunapelekeshwa na matakwa yetu na ubinafsi wetu si kama anavyotaka Mungu. Namna hii ya kutangatanga haitupatii utulivu na amani ya kweli na matokeo yake ni kushindwa kumuona Mungu katika mwanga wa ukweli.
Mtume Paulo katika Somo la Pili anatuonesha hadhi tunayokuwa nayo katika Kristo: “… kusudi walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao.” Ni mwaliko wa kuenenda zaidi katika namna ya roho, kujiunganisha na Mungu katika ukweli wote kama njia pekee ya kuuona uwepo wake hata unapokumbana na changamoto za kimaisha. Ni mwaliko wa kuepuka kishawishi cha kumwamini Mungu pale tu unapoyaona unayohitaji na kutamani yanafanikiwa na vinginevyo unashindwa kuuona uwepo wake. Mungu yupo nawe nyakati zote na mafanikio ya kweli ni kuuhisha daima uwepo wake ndani yako. Unapoanza kufanya lolote kwa ajili ya kujifanikisha au kujinufaisha wewe na si kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu na kwa ajili ya wokovu wako hapo ndipo utashindwa kuona uwepo wake pale unapodhania umekwama.
Inua macho yako kwa Bwana na jitegemeze kwake. Yeye anakutazama daima na hatokutupa. Yeye ambaye amekuumba amekuwekea yote mema kadiri ya mpango wake. Utafute mpango wake na mtimizie nadhiri zako kwako.
SALA: Ee Mungu utujalie moyo thabiti hasa katika dhoruba za maisha.