Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 08/06/2024
2024 JUNI 8 : JUMAMOSI-JUMA LA 9 LA MWAKA
MOYO SAFI WA BIKIRA MARIA
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 3
Somo 1. Isa 61: 9-11
Kizazi chao kitajuiikana katika mataifa, na uzao wao katika kabila za watu; wote wawaonao watakiri ya kuwa wao nikizazi kilicho barikiwa na Bwana. Nitafurahia Sana katika Bwana, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu. Maana Kama inchi itoavyo machipuko yake, na kama bustani ioteshavyo vitu vilivyopandwa ndani yake; ndivyo Bwana Mungu atakvyo otesha haki na sifa mbele ya mataifa yote. |
Wimbo wa Katikati. 1 Sam 2: 1, 4-8
1. Moyo wangu wamshangilia Bwana, (K) Moyo wangu wamshangilia Bwana. 2. Pinde zao mashujaa zimevunjika, 3. Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; 4. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, |
Injili. Lk 2: 41 – 51
Wazee wa Yesu huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyo desturi ya sikukuu; na walipokwisha kutimiza ile siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao, na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Nao walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, kwa nini kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu. |
TAFAKARI
TUWEKEE BIDII YA KUMTAFUTA YESU: Wahenga walisema uchungu wa mwana aujuae mzazi. Katika Injili ya leo tumesikia jinsi wazazi wa Yesu walivyokuwa na mahangaiko ya kumtafuta Yesu baada ya kutambua kuwa hakuwa pamoja nao tena katika safari yao. Hivyo walichukua maamuzi ya kumtafuta na baada ya siku tatu walimkuta hekaluni. Neno hili linatufundisha umuhimu wa kumtafuta Yesu kila dakika ya maisha yetu. Tusiruhusu kukaaa bila Yesu kwenye maisha yetu. Tangu tulipobatizwa tumekuwa kwenye safari moja na Kristo, na wakati mwingine tunampoteza kwa sababu ya dhambi zetu. Tusimsubiri yeye aje kututafuta kwani tayari alishatupa njia ya kumtafuta tunapompoteza. Tumtafute kwa njia ya Sakramenti ya upatanisho, kwa njia ya kupokea Ekaristi Takatifu, kwa njia ya Neno lake na kwa mafundisho yake. Tuwe na utaratibu mzuri wa kuwa na tafiti moyo za mara kwa mara ili tuchunguze kama bado tupo na Yesu au tumempoteza katikati ya wingi wa vita vya ulimwengu huu katika mambo ya kiroho. Tuige fadhila za Maria na Yosefu kumtafuta Yesu ayatawale maisha yetu. Sala: Ee Mama Bikira Maria utusaidie kumtafuta Yesu katika maisha yetu. |