Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 07/06/2024

2024 JUNI 7 : IJUMAA-MOYO MTAKATIFU WA YESU

MOYO MTAKATIFU WA YESU
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya Siku

Somo 1. Hos 11:1b, 3-4,8c-9

Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri. Lakini nalimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; naliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa naliwaponya. Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayari mwao, nikaandika chakula mbele yao. Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja. Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitarudi kumwangamiza Efraimu; kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya mji.

 

Wimbo wa Katikati. Isa 12: 2-6

1. Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
Nitatumaini wala sitaogopa;
Maana Bwana Yehova ni nguvu zangu
Na wimbo wangu;
Basi, kwa furaha mtateka maji
Katika visima vya wokovu.

(K) Basi, kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu.

2. Na katika siku hiyo mtasema,
Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,
Litajeni jina lake kuwa limetukuka. (K)

3. Mwimbieni Bwana, kwa kuwa ametenda makuu;
Na yajulikane haya katika dunia yote.
Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K)

Somo 2. Efe 3:8-12, 14-19

Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; na kwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote; ili sasa, kwa njia ya Kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu. Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini. Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa, wajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake, katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu. Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele.

Injili. Yn 19: 31-37

Wayahudi, kwa sababu ni maandalio, miili isikaaye juu ya misalaba siku ya Sabato (maana Sabato ile ilikuwa siku kubwa) walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe. Basi askari wakaenda wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulubiwa pamoja naye. Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; Lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; Na mara ikatoka damu na maji. Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; Naye anajua ya kuwa anasema kweli ili nyinyi nanyi mpate kusadiki. Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie, Hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na tena andiko lengine lanena, Watamtazama yeye waliyemchoma.

TAFAKARI

MOYO MTAKATIFU WA YESU, UFALME WAKO UFIKE: Tunapoadhimisha Sikukuu hii tunasherehekea ukuu wa upendo wa Mungu kwa wanadamu. Upendo ule ambao ulimsukuma Mungu ambaye “aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwanawe ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uhai wa milele”(Yn 3:16). Huu ndio upendo ambao ulimsukuma Kristo, Mchungaji Mwema autoe uhai wake kwa ajili ya kondoo wake (rej. Yn 10:11). Ni kwa upendo huo hata alipokuwa msalabani Yesu aliweza kuwasamehe watesi wake: “Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalolifanya”(Lk 23:34). Na kwa msamaha huo, upendo huwafikia hata wale ambao ni adui zetu. Kristo ametufundisha akisema”… Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni”(Lk 6:27). Ni sherehe ya kuzaliwa Sakramenti za Kanisa zilizotokana na ubavu wa Kristo uliochomwa kwa mkuki. “Askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji” (Yn 19:34). Moyo Mtakatifu wa Yesu ni shule yetu ya upendo; ni shule ya huruma ya Mungu; ni shule ya ukarimu na kujitoa mwili na roho kwa ajili ya wengine. 
SALA: Ee Yesu utujalie tuwe na bidi katika Ibada kwa Moyo wako Mtakatifu.