Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 03/06/2024

2024 JUNI 3 : JUMATATU-JUMA LA 9 LA MWAKA

Mt. Karoli Lwanga na wenzake Mashahidi
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Juma 4

Somo 1. 2 Pet 1:2-7

Neema na iwe kwenu na amani iongezwe katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu. Kwa kuwa uweza wake na Uungu wake umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa. Naam, kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo.

Wimbo wa Katikati. Zab 91: 1-2, 14-16

1. Aketiye mahali pa siri pake aliye juu
Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu,
Mungu wangu ninayemtumainia.

(K)Mungu wangu ninakutumaini.

2. Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu.
Kwa kuwa amekaza kunipenda
Nitamwokoa; na kumweka palipo juu,
Kwa kuwa amenijua jina langu.
Ataniita nami nitamwitikia, (K)

3. Nitakuwa pamoja naye taabuni,
Nitamwokoa na kumtukuza;
Kwa siku nyingi nitamshibisha,
Nami nitamwonesha wokovu wangu. (K)

Injili. Mk 12:1-12

Yesu alisema na Mafarisayo kwa mifano; “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akazungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Hata kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu. Wakamtwaa, wakampiga, wakamtoa nje, hana kitu.  Akatuma tena kwao mtumwa mwingine, na huyo wakamtia jeraha za kichwa, wakamfanyia jeuri.  Akamtuma mwingine, huyo wakamwua; na wengine wengi, hawa wakiwapiga na hawa wakiwaua.  Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, ‘Watamstahi mwanangu.’ Lakini wale wakulima wakasemezana, ‘Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu.’  Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu. Basi atafanyaje yule bwana wa shamba la mizabibu? Atakuja na kuwaangamiza wale wakulima, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Hata andiko hili hamjalisoma, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni. Neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu?” Nao wakatafuta kumkamata, wakaogopa mkutano; maana walitambua ya kwamba ule mfano amewanenea wao.  Wakamwacha wakaenda zao.

TAFAKARI

MUNGU ANAWAJALI WATU WAKE: Tumesikia mfano wa shamba la mzabibu. Mfano huu unatuonesha kuwa Mungu anawaandaa watu wake mwenyewe kama mtu anavyoandaa shamba lake. Anawabariki na kutaka wawe waaminifu kwake. Wanapokosa uaminifu Mungu anawatuma wajumbe kuwakumbusha wawe waaminifu. Tangu Agano la Kale Mungu aliwatumia Manabii kuwakumbusha watu kutunza maagano yao na Mungu. Baada ya Manabii hao wote Mungu alimtuma Mwanae pekee Yesu Kristo tumsikilize. Badala ya kumsikiliza, baadhi ya watu na hasa viongozi wa kidini na kijamii hawakumsikiliza wakafanya mipango ya kumwangamiza. Tuwe watu wa shukrani kwa kupokea misaada mbalimbali ya kiroho inayowekwa mbele yetu. Tuwe na unyenyekevu wa kupokea wajumbe wa Mungu wanaotumwa kwetu. Tuepuke hila dhidi ya wajumbe wa Mungu wanaotumwa kwetu. Tusiwaue kwa kusema mabaya juu yao au kwa kuharibu sifa zao njema. Badala ya kutafuta kuwaangamiza tushikrikiane nao vizuri kufanya kazi ya Mungu.

SALA: Ee Mungu tunakuomba utujalie moyo wa kuwapokea wajumbe wa habari njema unaowatuma kwetu.