Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 02/06/2024

2024 JUNI 2 : JUMAPILI-DOMINIKA YA MWILI NA DAMU TAKATIFU YA B. W. YESU KRISTU

Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya Siku

Somo 1. Kut 24: 3-8

Musa alienda akawaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema; akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli, akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng’ombe. Musa akatwaa nusu ya ile damu, akatia katika mabakuli; na nusu ya ile damu, akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyiza watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote.

Wimbo wa Katikati. Zab 116: 12-13, 15-18

1. Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha wokovu;
Na kulitangaza jina la Bwana.

(K) “Nitakipokea kikombe cha wokovu; Na kulitangaza jina la Bwana. “

2. Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake.
Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
Umevifungua vifungo vyangu. (K)

3. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
Na kulitangaza jina la Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote. (K)

Somo 2. Ebr 9: 11-15

Kristo aliisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. Kwa maana ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng’ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai? Na kwa sababu hii ni mjumbe wa agano jipya, ili, mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya agano la kwanza, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele. 

Injili. Mk 14: 12-16, 22-26

Siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile pasaka? Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini; atakutana nanyi mwanamume amechukua mtungi wa maji; mfuateni; na po pote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, Ki wapi chumba changu cha wageni, niile pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu? naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa, imeandikwa tayari; humo tuandalieni. Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka. Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa akisema, Twaeni; huo ndio mwili wangu. Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote. Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. Amin, nawaambia ninyi, sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu. Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda mlima wa Mizeituni.

TAFAKARI

EKARISTI TAKATIFU NI UZIMA WETU
Ni sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni Sikukuu ya Ekaristi Takatifu. Katekesimu ndogo ya mafundisho ya Komunyo ya kwanza yatufundisha kwamba Ekaristi ni Yesu mwenyewe mwenye kuwako katika maumbo ya mkate na divai. Ekaristi ni kumbukumbu iliyo hai ya karamu ile ya Yesu na wanafunzi wake ambapo walipokuwa wakila aliwaambia Huu ndio Mwili wangu; na hii ndio Damu yangu… Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi. (rej. Lk 22:19-21).
Ekaristi ni manna mpya. Inatukumbusha chakula kile walichokula Waisraeli kule jangwani, walipokuwa safarini kutoka utumwani Misri kuelekea Nchi ya Ahadi. (rej. Kut 16). Kama manna ilivyokuwa chakula cha wasafiri, kadhalika Ekaristi ni chakula cha wasafiri (Sisi) walio safarini kuelekea Nchi mpya ya Ahadi, mbinguni. Ekaristi hutupatia nguvu ya kiroho kuendelea na safari hiyo bila kukata tamaa.
Ekaristi ni utimilifu wa sadaka za Agano la Kale ambapo wanyama walichinjwa ili kumtolea Mungu sadaka. “…walitoa sadaka za kutekezwa, Wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng’ombe.”(Kut 24:5). Ukamilifu wa Agano la Kale umekamilika katika sadaka ya Kristo pale mlimani Kalvari. Ekaristi ni sadaka ya Kristu mwenyewe kujitoa Mwili na Damu yake kwa ajili yetu sisi na kwa ajili ya wengi. (Mk 14:24).
Ekaristi ni kiini na kilele cha maisha yetu ya kiroho, maisha ambayo hayana budi kuanzia na kuhitimishwa katika fumbo la Ekaristi Takatifu. Na kwa kutambua hilo, Ekaristi hutuunganisha sote. Ni kiini cha upendo na kifungo cha umoja. Mt. Paulo anatufundisha akisema “Kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili mmoja; maana sote twashiriki mkate huohuo”(1Kor 10:17). Na chanzo cha umoja huu ni Yesu mwenyewe asemaye “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake “(Yn 6:56).
Ekaristi Takatifu ni dawa ya kutokufa. Ni dawa ya uzima wa milele.  Yesu anasema “Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa Mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uhai ndani yenu. Anayekula mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uhai wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho. Maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli”(Yn 6:53-55).
Leo Mama Kanisa anawaalika watoto wake kumwabudu Yesu wa Ekaristi kwa namna ya pekee inayosindikizwa kwa nyimbo za shangwe wakifanya maandamano (kwa sehemu zile ambazo hufanya maandamano ya Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo) kwenye miji, vijiji na mitaa mbalimbali ili kumpeleka Kristo kwa watu awabariki na kuibariki miji yao. Lakini pia Wakristo Wakatoliki hutumia fursa hiyo ili kuutangazia ulimwengu fumbo lile wanalolikiri na kuliishi. Ni siku maalumu ya kuuambia ulimwengu kwamba Yafichikayo machoni imani huyaona.
Maandamano tuyafanyayo leo yanamdhihirisha Yesu wa Ekaristi kuwa ni Kuhani, Mfalme na Nabii. Ni Mfalme wa wafalme; ni Kuhani milele kwa mfano wa Melksedeki. Tunapoandama kumshangilia Yesu wa Ekaristi, tuipelekee dunia amani kwa kuwa Yesu anapita kwenye mitaa yetu akiwa ni Mfalme wa amani; tuipelekee dunia upendo kwani Mungu ni upendo; tuipelekee dunia matumaini kwani watu wamekata tamaa. Lakini zaidi sana tuitangazie dunia imani yetu katika Yesu wa Ekaristi. Kama Mungu alivyowalisha Waisraeli kwa unono wa ngano (Zab 80:17) na alivyowalisha kwa manna kule jangwani, tumwombe Kristo atulishe daima kwa chakula cha kweli, Ekaristi Takatifu. Ninawatakieni nyote Sherehe njema na Mungu atubariki sote.

SALA: Ee Yesu utulishe daima kwa chakula kitokacho mbinguni.