Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 01/06/2024

2024 JUNI 1 : JUMAMOSI-JUMA LA 8 LA MWAKA

Mt. Yustino, Shahidi
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Juma 3

Somo 1. Yud 1:17, 20-25

Wapenzi, yakumbukeni maneno yaliyonenwa zamani na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo, Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu, jilindeni katika Upendo wa Mungu, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo, hata mpate uzima wa milele. Wahurumieni wengine walio na shaka, na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili. Yeye awezaye kuwalinda ninyi msijikwae, na kuwasimamisha mbele ya utukufu wake bila mawaa katika furaha kuu; yeye aliye Mungu pekee, Mwokozi wetu kwa Yesu Kristo Bwana wetu; utukufu una yeye, na ukuu, na uwezo, na nguvu, tangu milele, na sasa, na hata milele. Amina.    

Wimbo wa Katikati. Zab 63:2-6

1. Ee Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema,
Nafsi yangu inakuonea kiu,
Mwili wangu wakuonea shauku,
Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.

Nafsi Yangu inakuonea kiu, Ee Bwana. (K)

2. Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu,
Nizione nguvu zako na utukufu wako.
Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai;
Midomo yangu itakusifu. (K)

3. Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai;
Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.
Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono;
Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha. (K)

Injili. Mk 11:27-33

Yesu na wanafunzi walifika Yerusalemu; alipokuwa akitembea hekaluni, walimwendea wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee, wakamwambia, Ni kwa mamlaka gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa mamlaka hii uyatende haya? Yesu akawaambia, Nitawauliza neno moja, nanyi mnijibu, kisha nitawaambia ni kwa mamlaka gani nayatenda haya. Ubatizo wa Yohane ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Nijibuni. Wakasemezana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema, Ulitoka mbinguni, atasema, Mbona, basi, hamkumwamini? Ila tukisema, Ulitoka kwa wanadamu. Waliogopa watu; maana watu wote walimwona Yohane kuwa nabii halisi. Wakamjibu Yesu, wakasema, Hatujui. Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani nayatenda haya.

TAFAKARI

YESU NDIYE MWENYE MAMLAKA YOTE: Katika Injili ya leo Yesu anahojiwa juu ya mamlaka ya kutenda aliyokuwa anatenda. Katika kujibu swali hili Yesu anawauliza mamlaka ya Yohani ya kubatiza yalitoka wapi. Swali la Yesu liliwagusa sana kwani ni kama linauliza wanataka kuwa chini ya uangalizi wa Mungu au chini ya uangalizi wa Mwanadamu? Wahenga “walisema penye ukweli uongo hujitenga.” Hawa walimwuliza Yesu swali ambalo walikuwa na jibu wakataka kumtega tu ila walishindwa kuusimamia mtego wao. Yesu anatufundisha juu ya mamlaka yake juu yetu, kuwa siyo umiliki wa kugandamizana bali ni wa upendo. Ninapotafakari mamlaka ya Yesu juu yangu ni lazima nimjibu Yesu. Yesu aliwaambia jibuni. Hii inamaanisha hatuwezi kuwa na jibu sahihi bila uwepo wa kusikia na kusikiliza kwa unyenyekevu. Hawa walishindwa kutoa jibu kwa sababu walisukumwa na hila na hivyo penye hila hamna mafanikio ya kweli. Tujiulize ndani ya mioyo yetu tuna mgawanyiko unaoleta uadui na Yesu?  Sasa kwa kutafakari uabatizo wetu tushinde mgawanyiko huo tubaki salama.

Sala: Ee Yesu unijalie neema na nguvu ya kukiri mamlaka yako.