Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 31/05/2024

2024 MEI 31 : IJUMAA-JUMA LA 8 LA MWAKA

BIKIRA MARIA KWENDA KUMWAMKIA ELIZABETI
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama Sala ya Siku

Somo 1. Sef 3:14-18

Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele Ee Israeli; furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu. Bwana ameziondoa hukumu zako, amemtupa nje adui yako; mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; hutaogopa uovu tena. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; atakushangilia kwa furaha kuu, atatulia katika upendo wake. Atakufurahia kwa kuimba.

Wimbo wa Katikati. ” Isa 12:2-6″

1. Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
Nitatumaini wala sitaogopa;
Maana Bwana Yehova ni nguvu zangu na wimbo wangu;
Naye amekuwa wokovu wangu.
Basi, kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu.

(K)Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.

2. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,
Litajeni jina lake kuwa limetukuka. (K)

3. Mwimbieni Bwana; kwa kuwa ametenda makuu;
Na yajulikane haya katika dunia yote.
Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K)

Injili. Lk 1:39-56

Mariamu aliondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti.  Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa  nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana. Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu,   Na jina lake ni takatifu. Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi  Kwa hao wanaomcha. Amefanya nguvu kwa mkono wake;  Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; Kama alivyowaambia baba zetu,  Ibrahimu na uzao wake hata milele. Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, Kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.

TAFAKARI

UPENDO KWA JIRANI: Leo ni sikukuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti. Injili inaelezea tukio hilo la Maria kumtembelea binamu yake Elizabeti. Wahusika wakuu katika Injili ni Bikira Maria na Elizabeti ambao wana kitu cha pekee cha kuelezea kuhusu mpango wa Mungu kwao. Wote wametumika kukamilisha mpango wa Mungu usio wa kawaida kwa mwanadamu. Maria alipoenda kwa Elizabeti alikuwa amembeba Yesu tumboni mwake na hivyo alipofika kwa Elizabeti alileta furaha kwake na kwa mtoto aliyekuwa tumboni kwa Elizabeti. Tunapowatembelea rafiki zetu tuwapelekee furaha katika familia zao. Tuoneshe upendo wa dhati kwao. Bikra Maria aliona Elizabeti alikuwa mhitaji kwa wakati ule na hivyo akafunga safari kwenda kumsalimia ili amsadie pia katika mahitaji yake ya wakati ule. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kuona mahitaji ya ndugu zetu ili tuwasaidie na tuweze kuwa sehemu ya furaha na baraka kwao. Yesu anapotutembelea kupitia watu au matukio mbalimbali tuwe tayari kumpokea kwa furaha.

Sala: Ee Yesu utujalie moyo wa kuwajali wengine.