Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 29/05/2024
2024 MEI 29 : JUMATANO-JUMA LA 8 LA MWAKA
Mt. Maximini
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 3
Somo 1. 1 Pet 1:18-25
Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo. Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu; ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu. Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo. Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele. Maana, Mwili wote ni kama majani, Na fahari yake yote ni kama ua la majani. Majani hukauka na ua lake huanguka; bali neno la Bwana hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu. |
Wimbo wa Katikati. Zab 147: 12-15, 19-20
1. Msifu Bwana, Ee Yerusalemu; (K)Msifu Bwana ee Yerusalemu. 2. Ndiye afanyaye amani mipakani mwako, 3. Humhubiri Yakobo neno lake, |
Injili. Mk 10:32-45
Walikuwako njiani, huku wakipanda kwenda Yerusalemu; na Yesu alikuwa akiwatangulia; wakashangaa, nao katika kufuata wakaogopa. Akawatwaa tena wale Thenashara, akaanza kuwaambia habari za mambo yatakayompata, akisema, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi, nao watamhukumu afe, watamtia mikononi mwa Mataifa, nao watamdhihaki, na kumtemea mate, na kumpiga mijeledi, na kumwua; na baada ya siku tatu atafufuka. Na Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, wakamwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lo lote tutakalokuomba. Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini? Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako. Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi? Wakamwambia, Twaweza. Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari. Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohane. Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi. |
TAFAKARI
TUMWIGE YESU KATIKA KUTUMIKIA: Leo katika Injili Yesu anazungumza tena juu ya kifo chake na hili linaleta malumbano kati ya wanafunzi wake kuwa ni nani aliye mkubwa kati yao. Hii inaonesha kuwa hata baada ya wanafunzi kukaa na Yesu kwa muda mrefu hawakubadili mtazamo wao wa kuona vitu. Yesu anawafundisha wao na sisi kuwa, ukubwa upo katika kutumikiana na siyo katika kutumikiwa. Yeye ndiye kielelezo cha utumishi ndiyo maana aliwaosha miguu na kuwataka nao wafanye hivyo pia. Ukubwa unaambatana na maisha ya kujitoa sadaka. Kikombe na ubatizo anaozungumzia Yesu ni ile sadaka ya kimasiha ambayo aliitoa kwa ajili ya ukombozi wa wengi. Hivyo anatutaka nasi kuwa wanyenyekevu na kuvaa hali ya utumishi na kuhudumia kwa upendo na siyo kutanguliza madaraka mbele. Utumishi kwanza mengine baadaye. Tutumie vizuri nafasi tulizo nazo ili kuhudumia watu wa Mungu. Utumishi huu ujikite siyo katika kumtumikia Yesu tu bali kwa wote kwani utumishi wa Yesu ulikuwa kwa watu wote bila ubaguzi. Sala: Ee Yesu nijalie moyo wa kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. |