Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 26/05/2024

2024 MEI 20 : JUMAPILI-UTATU MTAKATIFU

Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya Siku

Somo 1. Kum 4:32-34, 39-40

Musa aliwaambia makutano: Uliza sasa siku zilizopita, zilizokuwa kabla yako, tangu siku ile Mungu aliyoumba mwanadamu juu ya nchi, na toka pembe hii ya Mbingu hata pembe hii, kwamba kumetukia neno lolote kama hili kubwa, au kwamba kumesikiwa habari ya neno kama hili? je! watu wakati wowote wamesikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama wewe ulivyosikia, wasife? Au Mungu amekwenda wakati gani akajitwalia taifa toka kati ya taifa lingine, kwa majaribu, na kwa ishara, na kwa maajabu, na kwa vita, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa maogofya makuu, kama vile Bwana, Mungu wenu, alivyowatendea ninyi katika Misri, mbele ya macho yenu? Kwa hiyo ujue, leo hivi ukaweke moyoni mwako, ya kuwa Bwana ndiye Mungu katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana mwingine. Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele. 

WIMMBO WA KATIKATI. Zab 33:4-6, 9, 18-20, 22

1. Kwa kuwa neno la Bwana ni adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Bwana huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana.

(K)Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.

Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.
MaanaYeye alisema, ikawa;
Na Yeye aliamuru, ikasimama. (K)

3. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)

4. Nafsi zenu zinamngoja Bwana,
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tulivyokungoja Wewe. (K)

Somo 2. Rum 8:14-17

Kila mtu anayeongozwa na Roho wa Mungu, Huyo ndiye mtoto wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena Roho ya utumwa iletayo hofu; Bali mlipokea Roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, aba, yaani, baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithi pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.

Injili. Mt 28:16-20

Wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilaya, mpaaka mlima ule aliowaagiza Yesu. Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka. Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote Mbinguni na Duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza, kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu, na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.  

TAFAKARI 

TUMEUMBWA KATIKA SURA NA MFANO WA UTATU MTAKATIFU
Imani yetu imejengwa katika msingi huu: Tunaamini katika Mungu mmoja aliye katika nafsi tatu, yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Kanisa linatufundisha kwamba mgawayiko huu wa nafsi hujidhihirisha katika kazi zao: Baba ndiye muumbaji, Mwana ni mkombozi na Roho Mtakatifu ni mfariji. Utangulizi wa Ekaristi wa Sherehe ya Utatu Mtakatifu unaeleze kwa kifupi imani hiyo ukisema: “Wewe (Baba) pamoja na Mwanao wa pekee na Roho Mtakatifu u Mungu mmoja na Bwana mmoja, siyo katika umoja wa nafsi, ila katika utatu wa Mungu mmoja.” Nafsi hizi tatu katika umungu mmoja zina utukufu ulio sawa na kamwe hazigawanyiki. Hii ndiyo imani yetu, imani ambayo tunapaswa kuiungama kwa fahari.
Ufunuo wa Mungu unatufumbulia asili hii ya Mungu. Maandiko matakatifu yametudokeza juu ya fumbo hili la Mungu ambalo limejifunua kwa njia ya upendo wake mkubwa kwa wanadamu. Manabii waliuonesha upendo huo mkubwa wa Mungu na kwa ufunuo wa namna ya juu zaidi ni katika Kristo aliye ukamilifu wa ufunuo wa Baba na kwa kumshusha Roho Mtakatifu, msaada wetu katika kuzitambua siri na utajiri wa ufalme wa mbinguni. Ufunuo wa Mungu kwetu ni tendo linalosukumwa na upendo wake kusudi kutuelekeza sisi wanadamu katika njia sahihi na kuimarisha mahusiano mema na Yeye ili tusipotee. Kristo anamwambia Nikodemo juu ya upendo huo wa Mungu: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanae wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee.” Fumbo la Ukombozi linamfanya Kristo kuwa ufunuo wetu na kielelezo kwetu cha jinsi tunavyotakiwa kumfunua Mungu aliyeiweka chapa ya sura yake ndani mwetu.
Kristo anatanabaisha haiba yake, jinsi anavyohusiana na Mungu Baba, yaani anavyohusiana naye kama Baba na anakwenda mbali zaidi kutuambia sababu za ufunuo huo ni kumfanya mwanadamu asipotee. Sehemu ya Injili inatuambia kwamba “amwaminiye yeye (Mwana wa Mungu) haukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.” Msingi wa imani hii unajengeka katika asili hiyo ya Mungu. Neno kubwa tunalolionesha katika Sherehe ya Utatu Mtakatifu ni imani yetu katika Utatu Mtakatifu. Sehemu hii ya Injili inatuelekeza kwamba imani yetu katika Mwana wa Mungu, yaani katika ukweli juu ya asili yake na hivyo juu ya kazi zake zote alizofanya kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu ndiyo njia ya kujishikamanisha vyema na Mungu na hivyo kuepuka kuhukumiwa. Imani yetu katika Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu ndiyo inatuunganisha na fumbo la Utatu Mtakatifu sana unaofunuliwa kwetu kwa njia ya Kristo.
Wajibu wetu wakrirsto ni kuutambua utukufu wa Utatu Mtakatifu katika kuiungama imani ya kweli. Kuungama ni kuyakubali na kuyatekeleza yanayofunuliwa kwa njia ya Kristo, kuungama ni kuukubali utume wa Kristo ambao ulimuunganisha Mungu na mwanadamu. Wajibu huu unatuelekeza katika ushuhuda wa matendo yetu ya kimaadili ambayo yanatuunganisha sawasawa na Mungu. Imani yetu katika Utatu Mtakatifu si kwa maneno tu bali katika kazi zetu zinazochagizwa na ukweli huo. Ibada yetu ya kweli inaonekana katika mapinduzi ya kimaadili ambayo yatalifumbua fumbo hili la Utatu Mtakatifu kwa watu wote. Hapa ndipo tutakapowathibitishia na kuwaonesha watu wote juu ya tumaini letu. Hapa ndipo tutakapoidhihirisha sura ya Mungu ambayo kwayo mwanadamu ameumbwa.
Somo la kwanza la sherehe hii ya leo linatufunulia sifa za Mungu na namna ambavyo tunapaswa kushirikiana naye. Nabii Musa anamtaja kuwa ni “Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli.” Sifa hizo za kimungu zinauthibitisha upendo wake mkuu kwetu sisi wanadamu. Upendo wake mkuu unajidhihirisha katika fumbo la Ukombozi wetu, pale alipomtuma Mwanaye wa pekee ili kila amwaminiye awe na uzima. Hivyo ni Mungu ambaye hakai mbali na watu wake bali anawasogelea na anawaganga maovu yao; ni Mungu ambaye daima anasukumwa kunuia mema kwa watu wake. Hivyo, ushuhuda wetu wa chapa yake katika maisha yetu ni tendo la shukrani kwa Mungu wetu aliye karibu nasi kila tumwitapo. (rej. Kum 4:7).
Sehemu ya somo la kwanza inaendelea kutuambia kwamba: “Musa akafanya haraka, akainamisha kichwa chake hata nchi, akasujudu.” Amri ya kwanza ya Mungu inatutaka kutokuabudu miungu wengine. Bwana wetu Yesu Kristo alipojaribiwa na shetani kumsujudia alisema kwa ujasiri kabisa: “Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” Katika wimbo wa katikati wa liturujia ya leo tumesali tukisema: “Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.” Hapa tunaiona changamoto katika jamii yetu inayotuzunguka leo hii ambayo inamfanya Mungu kama «jambo la kawaida». Mwanadamu amepoteza uchaji na hofu ya Mungu na hivyo yupo katika hatari ya kutafuta kulinganisha matamanio na mivuto yake ya kidunia na ukuu wa Mungu.
Mara nyingi tunajidai kujua sana elimu juu ya Mungu lakini elimu hiyo hubaki kichwani tu. Ni aghalabu kuona katika matendo yetu leo hii tukimsujudu Mungu kama inavyostahili. Hii inadhihirisha kwamba pengine hata hatuna nafasi ya kutafakari nafasi yake na ukuu wake kwangu. Tujitafakari namna tunavyojisikia tuingiapo mahali patakatifu: Je, mavazi yetu yanamtukuza na kumsujudu Mungu? Je, akili na mawazo yangu nimeyaelekeza kwa Mungu? Mbona muda wote nafikiria simu yangu kwa kisingizio cha kufuatilia «dili» fulani? Mbona leo hii tunakurupusha amri zake na kujiwekea mambo yetu ambayo yatakidhi haja zetu? Tunamgeuza Mungu kama «mshikaji wetu»; hofu ya Mungu na uchaji hakuna na tunajikuta tunatumbukia katika vishawishi vya kutokuidhihirisha chapa ya sura yake iliyopo katika kila nafsi ya mmoja wetu.
Jamii yetu ya leo ambayo imegawanyika sababu ya vita, magomvi na kunyimana haki; ambayo imegawanyika katika matendo yanayokandamiza na kuharibu kabisa utu wa mtu inadhihirisha ukinzani kwa haiba ya kimungu aliye katika Utatu Mtakatifu. Mungu wetu katika Utatu Mtakatifu ni kielelezo cha umoja. Pale ninapotenda kukinzana na hitaji hili la umoja ni dhahiri kwamba siioni wala kuitambua nafasi ya Mungu kwangu na kujikinai kutenda yote kadiri nitakavyo mimi. Katika amani na uelewano Mungu anadhihirishwa. Tunamsujudu pale tunapotafuta amani na kuwatakia wengine uwepo wa Mungu katika Utatu Mtakatifu. Chapa ya sura yake imewekwa kwa wanadamu wote na hivyo tunapokutana na mwanadamu yeyote tunapaswa kudumisha umoja na mshikamano na kwa njia hiyo tutamtukuza na kusujudu Mungu katika ukweli.
Upendo wa Mungu umetufunulia haiba yake kwetu: Ni Mungu mmoja katika nafsi tatu. Tunapaswa kumtukuza na kumsujudu milele. Tumpatie nafasi yake inayostahili; tushirikiane naye katika namna inavyopaswa; tuimarishe imani yetu kwake kwa maana kwa njia hiyo ndipo tunaupokea wokovu. Tudumishe umoja kati yetu sisi kwa sisi kwa kuthamini utu wa kila mmoja wetu.

SALA: Ee Mungu utuzidishie imani juu ya Fumbo lako la Utatu Mtakatifu.