Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 25/05/2024

2024 MEI 25 : JUMAMOSI-JUMA LA 7 LA MWAKA

Mt. Beda, Mhashamu
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma

Somo 1. Yak 5: 13-20

Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinye; na mvua haikunya juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake. Ndugu zangu, ikiwa mtu wa kwenu amepotelea mbali na kweli, na mtu mwingine akamrejeza; jueni ya kuwa yeye amrejezaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu, ataokoa roho na mauti, na kufunika wingi wa dhambi.

Wimbo wa Katikati. Zab 141: 1-3, 8

1. Ee Bwana nimekuita, unijie hima,
Uisikie sauti yangu nikuitapo.
Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba,
Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.

(K)Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba.

2. Ee Bwana uweke mlinzi kinywani pangu,
Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.
Macho yangu yanakuelekea Wewe, Mungu Bwana,
Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu. (K)      

Injili. Mk 10: 13-16

Makutano walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.

TAFAKARI

TUWE SAUTI YA WASIO NA SAUTI: Katika Injili ya leo tumesikia Yesu ameletewa watoto, ila kwa sababu ambazo hazijaelezwa mitume wanawazuia watoto hawa. Yesu anawapa katekesi kuwa si sawa kuwazuia hawa watoto. Kwa katazo hili Yesu anatufundisha tuwe watetezi wa watoto na wanyonge. Watoto katika mtazamo huu wanaweza kuwa wachanga kiimani, waliotengwa na jamii kutokana na hali zao na wasiojiweza kwa ujumla. Hawa wanahitaji usaidizi wetu hivyo tusiwazuie. Badala ya kuzuia sauti za wanyonge tunapaswa kwa mwanga wa Injili kuwa sauti ya watoto na wanyonge katika jamii. Kipaumbele kwa ufalme wa Mbinguni ni kwa wale walio kama watoto kwa kuwa watoto hawana hila na wapo kama wanavyoonekana. Watoto daima ni wanyenyekevu na watiifu kwa wakubwa zao na wanaonesha kuwa tegemezi kwao. Nasi tuige fadhila za watoto hasa kutokuwa na hila na tuoneshe utegemezi wetu kwa Mungu. Kwa kuiga unyoofu wa watoto tutaurithi ufalme wa Mbinguni.

Sala: Ee Yesu tunaomba utujalie fadhila ya ujasiri ya kuwatetea walio wanyonge.