Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 23/05/2024
2024 MEI 23 : ALHAMISI-JUMA LA 7 LA MWAKA
Mt. Desideri wa Vienne, Askofu na Mfiadini
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma
Somo 1. Yak 5: 1-6
Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo. Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi. |
Wimbo wa Katikati. Zab 49: 14-15
1. Hiyo ndiyo njia yao, ujinga wao, (K)Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao. 2. Umbo lao linachakaa, kao lao ni kuzimu. 3. Usiogope mtu atakapopata utajiri, 4. Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai, |
Injili. Mk 9:41-50
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake. Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini. Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto. Chumvi ni njema; lakini chumvi ikiwa si chumvi tena, mtaitia nini ikolee? Mwe na chumvi ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi. |
TAFAKARI
TUSHINDE VISHAWISHI NA VILEMA VYETU: Injili ya leo inatufundisha kuwa ndani mwetu sote kuna vitu ambavyo vinaweza kuwa vizingiti au vizuizi katika kuishi ujumbe wa Habari Njema. Tunaalikwa leo kufahamu vizuizi hivi na kuviondoa. Yesu anaposema mkono au mguu ukikukosesha uukate au jicho likikukosesha ling’oe hamaanishi kutoa viungo hivi. Badala yake Yesu anatoa tahadhari tu kuondokana na mambo yale yanayokinzana na maisha yetu ya ufuasi. Yawezekana ni kilema fulani kama vile wivu, hasira, uchoyo, uvivu, masengenyo, tamaa mbaya na mambo mengine yasiyofaa. Hivi vyote ni vitu tunavyopaswa kuvikataa ili visiwe kizuizi kwetu. Yesu anatufundisha kuwa ukarimu unalipa kwani anayetoa msaada hata mdogo tu kwa ajili ya wahitaji hawatapungukiwa. Yesu anajali sadaka na majitoleo yetu mbalimbali tunayofanya kwa lengo la kuwezesha kazi yake. Hivyo tusichoke kujitoa kwa kazi za kanisa, tusichoke kulipa zaka, tusichoke kutenda mema. SALA: Ee Yesu utupe neema ya kushinda vilema vyetu vya kiroho. |