Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 22/05/2024

2024 MEI 22 : JUMATANO-JUMA LA 7 LA MWAKA

Mt. Rita wa Kashia
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma

Somo 1. Yak 4: 13-17

Haya basi, ninyi msemao, leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi. Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya. Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi.

Wimbo wa Katikati. Zab 49: 2-3, 6-8,10

1. Sikieni haya, enyi mataifa yote;
Sikilizeni, ninyi nyote mnaokaa duniani.
Watu wakuu na watu wadogo wote pia,
Tajiri na maskini wote pamoja.

(K)Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao.

2. Kwa nini niogope siku za uovu,
Ubaya ukinizunguka miguuni pangu?
Wa hao wanaozitumainia mali zao,
Na kujisifia wingi wa utajiri wao. (K)

3. Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake,
Wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake.
Maana fidia kuiacha hata milele
Wala hana budi kuiacha hata milele
Ili aishi sikuzote asilione kaburi. (K)

4. Naam, ataliona, hata wenye hekima hufa;
Mpumbavu na mjinga hupotea pamoja,
Na kuwaachia wengine mali zao. (K)

Injili. Mk 9:38-40

Yohane alimjibu Yesu akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi. Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu.

TAFAKARI

JINA LA YESU NI NGUVU YA WANAOMKIRI: Leo tumesikia Mitume wakimweleza Yesu kuwa wamemkataza mtu kutenda muujiza kwa jina lake kwa kuwa si mwanajumuiya mwenzao. Yesu anawapa katekesi kuwa anayetumia jina lake si mpinzani wake. Tunapaswa kuelewa kuwa nguvu ya Mungu haifungiwi sehemu moja tu. Mungu anatenda kazi kupitia yeyote ampendaye pasipo kujali dini yake. Yesu anasema wazi kuwa mtu anayemwamini ataweza kufanya mambo aliyofanya yeye hata mambo makubwa zaidi (rej. Yn 14:12). Tusioneane wivu Yesu anapogawa karama mbalimbali kwa watu mbalimbali. Tufurahi kuona kuwa kwa karama hizo Injili inahubiriwa na watu wanapata wokovu na tunashinda vita dhidi ya Ibilisi. Tusione wivu wenzetu wanapofanikiwa badala yake tufurahie mafanikio yao na kujifunza kwao ili tupate mafanikio pia. Hiki kilichotokea katika Injili kilishawahi kutokea tena katika Kitabu cha Hesabu (rej. 11:26-29) wakati Joshua alipomwomba Musa awakataze Eldadi na Medadi kutoa unabii. Jibu la Musa lilikuwa laiti Mwenyezi Mungu angewapa watu wake wote roho yake nao wawe manabii. 

Sala: Ee Yesu tunaomba utuepushe na wivu.