Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 21/05/2024
2024 MEI 20 : JUMANNE-JUMA LA 7 LA MWAKA
Christopher Magallanes
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 7
Somo 1. Yak 4: 1-10
Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu; mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu. Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu. Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu. Basi mtiini Mungu. Mpingeni shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza. |
Wimbo wa Katikati. Zab 55: 7-11, 23
1. Nikasema, Ningekuwa na mbawa kama njiwa, (K)”Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele. “ 2. Ningefanya haraka kusikimbia 3. Maana nimeona dhuluma na fitina katika mji 4. Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, |
Injili. Mk 9:30-37
Yesu na wanafunzi wake walipita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza. Wakafika Kapernaumu; hata alipokuwamo nyumbani, akawauliza, Mlishindania nini njiani? Wakanyamaza; kwa maana njiani walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa. Akaketi chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote. Akatwaa kitoto, akamweka katikati yao, akamkumbatia, akawaambia, Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma. |
TAFAKARI.
UKUBWA NI UTUMISHI: Injili ya leo inatangaza kwa mara ya pili kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Mitume waliogopa kwani hawakuwa na uelewa wa Masiha ambaye ni mtumishi wa wengine. Yesu anapowagusia kuhusu mateso yake wanaanza kujadili ni nani atakayekuwa mkubwa kati yao. Yesu anawafundisha na kutufundisha sisi kuwa ukubwa upo katika kuwahudumia wengine. Tukumbuke kuwa nafasi mbalimbali za uongozi zinapaswa kutushusha na kutufanya wanyenyekevu. Tutumie vizuri nafasi tulizopewa na jamii kwa kutoa huduma stahiki kwa wale tunaowahudumia. Zaidi sana tuwajali hasa wale wanaoonekana kuwa wadogo katika jamii. Tuwajali sana watu wa pembezoni katika kutoa huduma kwani kwa namna moja au nyingine wanamwakilisha Kristo. Tusijikite katika kuwahudumia watu wa tabaka la juu tu na kuwaacha watu wa tabaka la chini. |
Sala: Ee Yesu utujalie moyo wa kuhudumia zaidi kuliko kupenda kuhudimiwa. |