Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 16/04/2024

2024 APRILI 16 : JUMANNE-JUMA LA TATU LA PASAKA

Mt. Benedikto Yosefu Labre
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Mdo 7:51 – 8:1

Stefano aliwaambia wakuu wa Makuhani: Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote Mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo. Ni yupi katika manabii ambaye baba zenu hawakumwudhi? Nao waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki; ambaye ninyi sasa mmekuwa wasaliti wake, mkamwua; ninyi mliyoipokea torati agizo la malaika msiishike. Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno. Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu. Akasema, Tazama, naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu. Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.

(K) Mikononi mwako naiweka roho yangu, ee Bwana.

Wimbo wa Katikati. Zab 31:3cd, 4, 6, 7b, 8a, 17, 21ab

“1. Uwe kwangu mwamba wa nguvu,
Nyumba yenye maboma yakuniokoa.
Ndiwe genge langu na ngome yangu:
Kwa ajili ya jina lako uniongoze,unichunge. (K)

2. Mikononi mwako naiweka roho yangu:
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.
Bali mimi namtumaini Bwana.
Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako. (K)

3. Umwangaze mtumishi wako
Kwa nuru ya uso wako;
Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
Utawaficha katika hema
Na mashindano ya ndimi. (K)”

Injili. Yn 6:30-35

Siku ile, Wayahudi walimwambia Yesu: Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani? Baba zetu waliila mana jangwani, kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale. Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. Basi wakamwambia, Bwana, siku zote utupe chakula hiki. Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe.

TAFAKARI

UZIMA WA MBINGUNI UNAPALILIWA NA SALA: Wayahudi walipata fursa ya kukutana na Yesu mara nyingi na waliweza wakati mwingine kuuliza maswali ili kujiridhisha. Swali la leo la kutaka ishara na katika jibuu, Yesu kuwajibu kwa kuwawaonesha umuhimu wa mwili wake (Ekaristi Takatifu), kuwa ni kwa kula ipasavyo Ekaristi Takatifu tutaurithi uzima wa milele. Ukisoma 1Tim2:4 “Mungu anataka watu wote waokolewe na wapate kuujua ukweli”; ni katika kuujua ukweli tunaweza kujikita katika sala na kuweza kustahimili katika magumu kama Stefano alivyoweza. Stefano aliweza hata kutoa msamaha akilekea kwenda mbinguni. Ni kwa nguvu ya sala aliweza kutamka msamaha. Mtakatifu Yohani Chrisostom anasema “Kama ilivyo mwili bila roho ni maiti, ndivyo ilivyo kwa roho pasipo sala ni mfu.” Ni kwa kuishi maisha ya sala tutaweza kuelewa ujumbe huu wa Kristo kushuka toka mbinguni ili kutuokoa.

SALA: Ee Yesu tuwezeshe kukupokea ipasavyo katika meza ya Ekaristi Takatifu.