Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 13/04/2024

2024 APRILI 13 : JUMAMOSI-JUMA LA PILI LA PASAKA

Mt. Martino I, Papa na Shahidi
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 2

“…wakamwona Yesu anakwenda juu ya bahari na kukikaribia chombo; wakaogopa. Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope.”

Somo 1. Mdo 6:1-7

Siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung’niko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile neno. Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao. Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya Wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile imani.

K) “Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tulivyokungoja Wewe. “

Wimbo wa Katikati. Zab 33:1-2, 4-5, 18-19

“1. Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
Mwimbieni wimbo mpya,
Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe. (K)

2. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)

3. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)”

Injili. Yn 6:16-21

Jioni wanafunzi walitelemka baharini; wakapanda chomboni, wakaanza kuivuka bahari kwenda Kapernaumu. Nako kumekwisha kuwa giza, wala Yesu hajawafikia. Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu. Basi wakavuta makasia kadiri ya maili tatu nne, wakamwona Yesu anakwenda juu ya bahari na kukikaribia chombo; wakaogopa. Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope. Basi wakataka kumpokea chomboni; na mara hiyo chombo kikaifikilia nchi waliyokuwa wakiiendea.

TAFAKARI

UWEZA WA MUNGU NI MKUU: Kanisa Katoliki lina utaratibu kuwa mapadre hawaoi. Hii ni nidhamu iliyowekwa ili kuweza kuwapa fursa nzuri zaidi za kumtangaza Kristo kwa watu kwa uzuri na ufanisi bila kubanwa na shughuli za familia. Katika somo la kwanza, tumeona jinsi jamii ile ya mitume ilivyotoa ushauri wa kuwateua wachache miongoni mwa watu ili kuwapa mitume muda mzuri kwa kazi ya utumishi. Katika Injili tumeona Kristo anawatoa mitume wake hofu na kuandamana nao katika utume. Hapa tunaona wazi kuwa Yesu yuko daima na Kanisa katika utume wake, hata katika misukosuko haliachi liangamie, “Bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu.” Kanisa linapigwa vita vikali. Kitendo cha Kristo kukemea ule upepo, ni kuonesha ukuu na uweza wa Mungu katika kuandamana na Kanisa. Kamwe tusichoke na kuona kuwa tunashindwa, bali katika nguvu za Kristo mfufuka tunashinda.

SALA: Ee Kristo Mfufuka, ulilinde Kanisa lako dhidi ya dhoruba zote.