Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 12/04/2024

2024 APRILI 12 : IJUMAA-JUMA LA PILI LA PASAKA

Mt. Zeno, Askofu na Shahidi
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Mdo 5:34-42

Mtu mmoja, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo, akawaambia, Enyi waume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa. Kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu. Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote waliomsadiki wakatawanyika. Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu. Wakakubali maneno yake; nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao. Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya jina hilo. Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri Habari Njema za Yesu kwamba ni Kristo.

Wimbo wa Katikati. Zab 27:1, 4, 13-14

“1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani? (K)

K) “Neno moja nimelitaka kwa Bwana,
Nikae nyumbani mwa Bwana. “

2. Neno moja nimelipata kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana
Siku zote za maisha yangu.
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake. (K)

3. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)”

Injili. Yn 6:1-15

Wakati ule, Yesu alikwenda zake ng’ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akakwea mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyo ni nabii yule ajaye ulimwenguni. Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.

TAFAKARI

UKARIMU NI FADHILA NJEMA: Kutoa na kujitolea kwa ajili ya wengine ni tendo jema la kujisadaka linalohitaji maandalizi. Ni hali iliyojaa utu na huruma yenye upendo. Kutoa kwa ajili ya wengine bila upendo hakuna maana. Yesu alipowaona makutano wako katika uhitaji, aliwaonea huruma na akaanza maandalizi ya kuwahudumia kwa kuwashirikisha wanafunzi wake watoe walicho nacho. Yesu hakushindwa kufanya bila kuwahusisha wanafunzi wake, alifanya vile kwa makusudi mazima ili awajengee tabia ya kuendeleza hilo. Yesu alipochukua ile mikate ya yule kijana (na hatujaelezwa kama aliinunua au alimwomba) anatualika na sisi tugawane/tushirikishane tulivyo navyo. Kuna watu kujitolea kwa ajili ya wengine ni msamiati au hata akitoa basi anatoa kile asichokipenda, vibovu, chakavu n.k au anatoa na kutangza kwa wengine. Kukosa ukarimu kunatunyima Baraka nyingi. Wachagga wana usemi usemao “ukafuna kwa malele kyefumbuka” wakimaanisha kuwa ‘ukitoa kwa ukarimu kinaongezeka.’

SALA: Ee Yesu utupe moyo wa ukarimu.