Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 10/04/2024
2024 APRILI 10 : JUMATANO-JUMA LA PILI LA PASAKA
Mt. Magdalena wa Kanosa, Mtawa na Mwanzilishi wa Shirika
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 2
Somo 1. Mdo 5:17-26
Aliondoka kuhani mkuu na wote waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo), wamejaa wivu, wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza. Lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni mkasimame hekaluni, mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu. Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha. Akaja kuhani mkuu nao waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli, wakatuma watu gerezani ili wawalete. Hata watumishi walipofika hawakuwaona gerezani, wakarudi wakatoa habari, wakisema, Gereza tumeikuta imefungwa salama, nao walinzi wamesimama mbele ya mlango; lakini tulipoufungua hatukukuta mtu ndani. Basi jemadari wa hekalu na wakuu wa makuhani waliposikia haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao, litakuwaje jambo hilo. Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya kwamba, Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu. Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe.
Casula
CASULA...
Wimbo wa Katikati. Zab 34: 2-3, 4-9
“1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake si kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi. (K)
K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia.
2. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote. (K)
3. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote. (K)
4. Malaika wa Bwana hufanya kituo,
Akiwazungukia wamchao na kuwakoa.
Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema;
Heri mtu yule anayemtumaini. (K)
“
Injili. Yn 3:16-21
Yesu alimwambia Nikodemo: Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.
TAFAKARI
HAKIKA MUNGU NI MWEMA: Maelezo ambayo Yesu alimpatia Nikodemu yanadhihirisha jinsi gani Mungu alivyo mwema kwa wanadamu aliowaumba kwa sura na mfano wake, “kwa maana jinsi hii, Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanae wa pekee.” Kuja kwa Kristo ulimwenguni ni ili sisi tupate wokovu, hivyo yatupasa kumwamini, tuwe kweli nuru kwa wengine. Ni Kristo huyu ndiye aliyewawezesha mitume tuliosikia katika somo la kwanza kuweza kuwashinda wale waliotaka kuwakwamisha katika utume wao kwa kuwafunga gerezani. Baadhi ya sehemu nyingine Kanisa linapita katika upinzani mwingi, ardhi ya Kanisa kudhulumiwa, mapadre kufanyiwa vitendo vya kikatili kama kuuawa, waamini kukatishwa tamaa n.k. Lakini Neno la Mungu linatupa nguvu kwani alisema ‘atakayevumilia mpaka mwisho, ndiye atakayeokoka.’
SALA: Mungu Mwenyezi, saidia Kanisa lako katika mapambano na misukosuko ya ulimwengu.