Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 07/04/2024

2024 APRILI 7 : DOMINIKA YA HURUMA YA MUNGU
                                                                                
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

Somo 1. Mdo 4: 32-35
Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu chochote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika. Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji.

Wimbo wa Katikati. Zab 118:2-4, 13-15,22-24
“1. Israeli na aseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
Mlango wa Haruni na waseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
Wamchao Bwana na waseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele. (K)

(K) “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
kwa maana fadhili zake ni za milele. “

2. Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;
Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Sitakufa bali nitaishi,
Nami nitayasimulia matendo ya Bwana.
Bwana ameniadhibu sana,
Lakini hakuniacha nife. (K)

3. Jiwe walilolikataa waashi
Limekuwa jiwe kuu la pambeni.
Neno hili limetoka kwa Bwana,
nalo ni ajabu machoni petu.
Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana,
Tutashangilia na kuifurahia. (K)”

Somo 2. 1 Yoh 5: 1-6
Kila mtu aaminiye kwamba Yesu ni Kristo amezaliwa na Mungu. Na kila mtu ampendaye mwenye kuzaa, ampenda hata yeye aliyezaliwa na yeye. Katika hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu, tumpendapo Mungu, na kuzishika amri zake. Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito. Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu. Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu? Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo; si katika maji tu, bali katika maji na katika damu Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli.

Injili. Yn 20:19-31
Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu.

Naye akiisha kusema hayo, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.Naye akiisha kusema hayo, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi, Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa. Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. Basi, wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo. Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu. Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako, uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye. Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu! Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki. Basi, kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandiwa; ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.

TAFAKARI

“UPYA WA MAISHA YA KIPASKA UNARUTUBISHWA NA HURUMA YA MUNGU
Mtume Petro anatualika katika antifona ya mwanzo ya Dominika hii akituambia: “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu.” Tuuunganishe mwaliko huu na adhimisho la Huruma ya Mungu ambalo tunaalikwa katika Dominika hii ya pili ya Pasaka ambayo inahitimisha siku nane au Oktava ya Sherehe ya Pasaka. Maziwa yasiyoghoshiwa ni maziwa halisi ya mama ambayo hayajachanganywa na kitu chochote. Hii ni lishe muhimu kwa mtoto mchanga kwa ajili ya kumjengea kinga za asili na ambazo zinarandana na vinasaba vyake kutokana na ukaribu wa mama na mtoto wake. Inakuwa ni bahati mbaya kwa mtoto mchanga kukosa maziwa ya mamaye kwa sababu fulani kwani pia pamoja na kumpatia lishe na mengineyo ya kumkuza, kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama yake humuunganisha kwa karibu na mzazi wake.
Tangu zamani Kanisa pia inaiita dominika hii kwa jina la “in albis” ambayo iliunganishwa na ukamilifu wa ibada kwa wale waliobatizwa wakati wa mkesha wa Pasaka. Kila mkristo mpya alivishwa nguo nyeupe kuashiria mwanzo mpya na kupata hadhi mpya ya kuwa mwana wa Mungu. Nguo hiyo inapaswa kuvaliwa kwa juma zima hadi dominika ya leo ambapo nguo hiyo inatolewa. Hapa wanapewa sasa hadhi ya kuanza maisha mapya ndani ya Kanisa na kwa msingi huo maisha hayo yalipaswa kustawishwa na kanisa lenyewe kwa njia ya Sakramenti zake. Ndiyo maana wanaalikwa kuyatami mazima yasiyochakachuliwa, maziwa halisi kusudi kwa hayo wapate “wakate kuukuliwa wokovu”. Ni mwaliko wa kubaki katika mafundisho na misingi ya kanisa kwa makusudi ya kuufikia wokovu.
Dhana hiyo inaunganika vizuri na Huruma ya Mungu ambayo tunaalikwa kuiadhimisha leo. Kimsingi fumbo zima la Pasaka linaiadhimisha Huruma ya Mungu. Adhimisho la huruma ya Mungu lina asili yake tangu wakati wa adhimisho la Jubilei Kuu ya Mwaka 2000. Huruma ya Mungu inatuangaza kulielewa vema Fumbo la Pasaka kwani huzifungua akili zetu ili kulielewa vema fumbo la Mungu na uwepo wetu hapa duniani. Hivyo kutusukuma kuwa mashuhuda wa Pasaka katika maisha yetu. Hivyo huruma hiyo ya Mungu ambayo Mtakatifu Faustina Kowalska aliiona kama miale ya rangi ya nyekundu ikiwakilisha damu ya Kristo na rangi ya bluu hafifu iliyokwajuka au samawati ambayo iliwakilisha maji ya ubatizo yaliyozistahilisha tena roho za wanadamu mbele ya Mungu. Kwa hiyo adhimisho la Huruma ya Mungu huufunua ukarimu, msamaha na upendo wa Mungu ambao kwa ujumla wake huadhimishwa katika fumbo la Pasaka.
Injili ya Dominika hii hutupatia simulizi la Tomaso, mtume ambaye kwanza aliona shaka lakini alifunuliwa ubavu na Kristo mwenyewe na kuona aliishia katika kuamini. Ubavu wake Kristo uliofunuliwa unatufungulia hazina za ufalme wa Mungu na hayo ndiyo maziwa yasiyoghoshiwa tunayoalikwa kujishibisha nayo kwa ajili ya wokovu wetu. Tunapoelekeza macho yetu na kumtazama Yeye waliyemchoma ndipo tunapoonja urefu na upana wa upendo wa Mungu na hivyo kukiri kama Mtume Tomaso “Bwana wangu na Mungu wangu” na kisha kwenda kushuhudia kwa matendo yetu.
Pasaka inatupatia maisha mapya yanayochipuka katika Kristo mfufuka. Jumuiya ya kwanza ya Wakristo ilidhihirisha upya huu wa maisha katika maisha yao ya kindugu. Kwanza walikuwa na moyo mmoja na roho moja; hakuna ambaye alimiliki sana au kukosa kabisa. Wote waliishi katika hali ya umoja, “wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao aliyekuwa na mahitaji.” Furaha ya Kristo mfufuka inamsukuma kila mmoja kujiona anaungana na ndugu yake. Waliokuwa navyo wanajitoa na kuwagawia wengine. Hapa tunaona moja ya tunda muhimu linaloletwa na Kristo mfufuka, yaani kuwaunganisha wanadamu wote katika nafsi yake. Sote tunakuwa ni kaka na dada kwani kwa kuungana na Kristo tunafanywa kuwa mwili mmoja na roho moja. Muungano wetu huu katika Kristo unastawishwa na neema zake Kristo mwenyewe zinazobubujika kutoka ubavuni mwake.
Neema za Kristo zinazotububujikia kutoka ubavuni mwake ndizo zinazotuwezesha katika karama mbalimbali ambazo kwazo tunapaswa kuzidhihirisha kama jamii ya wakristo wa kwanza, yaani kwa ajili ya watu wote. Tumshuhudie Kristo kwa kufanya juhudi ya kuukarabati ubinadamu ulichakazwa. Hiyo ndiyo inapaswa kuwa alama ya jamii ya kikristo ambayo inapambwa na upendo.
Tukiwa tumepokea upya huu wa maisha ya kipasaka tuiadhimishe Pasaka hiyo katika maisha yetu huku tukichagizwa na baraka za kimbingu zinazotububujikia kutoka ubavuni mwa Kristo. Hizo ndizo neema mbalimbali zipatikanazo kwa njia ya huduma ya kanisa; ndiyo maziwa yasiyoghoshiwa ambayo kwayo tutaufikia wokovu.”

SALA: Ee Kristo Mfufuka, utujalie neema ya kukiri Ufufuko wako kama alivyofanya Mt. Tomaso Mtume.