Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 05/04/2024
2024 APRILI 5 : IJUMAA-JUMA LA KWANZA LA PASAKA Mt. Vinsenti Ferreri, Padre
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
Somo 1. Mdo 4:1-12
Petro na Yohane walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na akida wa hekalu na Masadukayo wakawatokea, wakifadhaika sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo wa wafu. Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni. Lakini wengi katika hao waliosikia lile neno waliamini; na hesabu ya watu waume ikawa kama elfu tano. Hata asubuhi wakubwa na wazee na waandishi wakakusanyika Yerusalemu, na Anasi kuhani mkuu, na Kayafa pia, na Yohane na Iskanda, na wote wale waliokuwa jamaa zake kuhani mkuu. Walipowaweka katikati, wakawauliza, kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya? Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema, alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.
Wimbo wa Katikati. Zab 118:1-2, 4, 22-27
1. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, (K) Jiwe walilolikataa waashi 2. Jiwe walilolikataa waashi 3. Ee Bwana, utuokoe, twakusihi; |
Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka.
Injili. Yn 21:1-14
Siku zile, Yesu alijidhihirisha tena kwa wanafunzi wake, penye bahari ya Tiberia, naye alijidhihirisha hivi. Simoni Petro, na Tomaso aitwaye Pacha, na Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, na wana wa Zebedayo, na wengine wawili wa wanafunzi wake, walikuwapo pamoja. Simoni Petro aliwaambia, Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe. Basi wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu. Hata asubuhi kulipokucha, Yesu alisimama ufuoni; walakini wanafunzi hawakujua ya kuwa ni Yesu. Basi Yesu akawaambia, Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, La! Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki. Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini. Nao hao wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata dhiraa mia mbili; huku wakilikokota lile jarife lenye samaki. Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate. Yesu akawaambia, Leteni hapa baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi. Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka. Yesu akawaambia. Njoni mfungue kinywa. Wala hakuna mtu katika wale wanafunzi aliyethubutu kumwuliza, U nani wewe? Wakijua ya kuwa ni Bwana. Yesu akaenda akautwaa mkate, akawapa, na samaki vivyo hivyo. Hiyo ndiyo mara ya tatu ya Yesu kuonekana na wanafunzi wake baada ya kufufuka katika wafu.
TAFAKARI
HUWEZI KUPINGANA NA MPANGO WA MUNGU: Yesu alimkabidhi Petro jukumu la kuendeleza na kusimamia Kanisa. Lakini tunaona anafika mahali anakata tamaa na kutaka kupingana na mpango huo na kurudia kazi yake ya awali. Mungu humwita kila mtu kwa wito fulani. Wapo baadhi wanajikuta wanaishi maisha ya mateso kwa sababu wanaingia katika wito ambao sio, labda kwa kuwaiga wenzao, hawatafakari kwanza kabla, hawamshirikishi Mungu, wanasikilizia nafsi zao tu, wanasahau kuwa Mungu ndiye anayeamua na kutaka wito fulani na kuwa kuna haja ya kumsikiliza yeye na sio vionjo vyao. Msikie Petro akisema “naenda kuvua samaki.” Hii ilimfanya asahau lile kundi alilokabidhiwa. Kuna sehemu nyingine tunashuhudia mapadre wanajihangaisha na biashara hadi kusahau utume wao, ofisini hawakai, hawaadhimishi hata sakramenti za Kanisa kama Ekaristi, Kitubio au kutoa mashauri kwa watu. Injili inatoa mkazo katika hili, kuwa hayo sio ya msingi. Petro pia anasimama kwenye nafasi ya kukumbusha viongozi kuwa imara ili wasiwapoteze wengine kwani wao ndio dira.
SALA: Ee Yesu tujalie ili tudumu katika miito yetu ulituita.