Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 22/03/2024

2024 MACHI 22 IJUMAA: JUMA LA 5 LA KWARESIMA
Mt. Deogratias, Askofu 
Urujuani
Zaburi: Juma 1

Somo 1. Yer 20:10-13

Nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki; huenda akahadaika; nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake. Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe. Lakini, Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu. Mwimbieni Bwana; msifuni Bwana kwa maana ameiponya roho ya mhitaji katika mikono ya watu watendao maovu. 

Wimbo wa Katikati. Zab 18:2-7

1. Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;
Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu
Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia,
Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.
Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa,
Hivyo nitaokoka na adui zangu. (K)

(K) Katika  shida yangu nalimwita Bwana,
      Akaisikia sauti yangu.


2. Kamba za mauti zilinizunguka,
Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.
Kamba za kuzimu zilinizunguka,
Mitego ya mauti ikanikabili. (K)

3. Katika shida yangu nalimwita Bwana,
Na kumlalamikia Mungu wangu.
Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake,
Kilio changu kikaingia masikioni mwake. (K)

Injili. Yn 10:31-42

Wayahudi waliokota mawe ili wampige. Yesu akawajibu, Kazi njema nyingi nimewaonyesha, zitokazo kwa baba; kwa ajili ya kazi ipi  katika hizo mnanipiga kwa mawe? Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu. Yesu akawajibu, Je!  Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu? Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka); je! yeye ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, Unakufuru; kwa sababu nalisema, Mimi ni Mwana wa Mungu? Kama sizitendi  kazi za Baba  yangu,  msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba. Wakatafuta tena kumkamata; lakini akatoka mikononi mwao. Akaenda zake tena ng’ambo ya Yordani, mpaka mahali pale alipokuwapo Yohane akibatiza hapo kwanza, akakaa huko. Na watu wengi wakamwendea, wakasema, Yohane kweli hakufanya ishara yo yote, lakini yote aliyoyasema Yohane katika habari zake huyu yalikuwa kweli. Nao wengi wakamwamini huko.

TAFAKARI

UKWELI UNAUMA: Mwanadamu hapendi kuelezwa ukweli na hasa pale ambapo inagusa vionjo vyake. Yesu alichukiwa na Wayahudi hadi kutaka kumpiga kwa mawe kutokana na yeye kuwaambia ukweli uliowachoma mioyo yao. Aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela alichukiwa na Makaburu hadi kufungwa gerezani kutokana na kuwaeleza ukweli juu ya kuwanyanyasa Waafrika kwa ubaguzi wa rangi. Sehemu nyingi tunakosa watu walio na ujasiri wa kusimamia ukweli, wengi wanabembeleza urafiki wa Kaisari, kupenda tu kusema yale yanayofurahisha vionjo vyao hata kama sio haki au ukweli. Kutoa hukumu bila haki, kuishi maisha ya ‘bendera fuata upepo’ kwa vile fulani kasema hivi na mimi naunga mkono. Kwamba “Wayahudi waliokota mawe ili wampige” inaonesha jinsi mtu anavyoweza kuhukumiwa na kundi bila haki. Watu wanaweza kupiga kelele, ‘mwizi mwizi’ na bila hata kuuliza kaiba nini, utasikia wengine wanadakiza, ‘piga ua, piga huyo ua’, mtu anauawa kwa makelele yasiyo na kiongozi. Haya ndiyo yaliyomkuta Yesu nyakati zake. Je! Hatuyatendi kama haya?

SALA: Ee Mungu utujalie kusimamia ukweli hata kama ni kuhatarisha maisha yetu.