Itukuzwe Damu ya Yesu. Karibu Katika Masomo ya Misa 12/02/2024
2024 FEBRUARI 12 JUMATATU: JUMA LA 6 LA MWAKA
Wat. Sirili, Mtawa, na Metodi, Askofu
Kumbukumbu
Nyeupe
Zaburi: Juma 2
Somo 1. Yak 1: 1-11
Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana wetu Yesu Kristo, kwa kabila kumi na mbili waliotawanyika; salamu. Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno. Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima na aombe dua kwa mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa. Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana. Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote. Lakini ndugu asiye na cheo na afurahi kwa kuwa ametukuzwa; bali tajiri kwa kuwa ameshushwa; kwa maana kama ua la majani atatoweka. Maana jua huchomoza kwa hari, huyakausha majani; ua lake huanguka, uzuri wa umbo lake hupotea; vivyo hivyo naye tajiri atanyauka katika njia zake.
Wimbo wa Katikati. Zab 119:67, 68, 71, 72, 75, 76
1. Kabla sijateswa mimi nalipotea,
Lakini sasa nimelitii neno lako.
Wewe U mwema na mtenda mema,
Unifundishe amri zako. (K)
(K) Rehema zako, Ee Bwana,
zinijie nipate kuishi.
2. Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa,
Nipate kujifunza amri zako.
Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
Kuliko maelfu ya dhabihu na fedha. (K)
3. Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki,
Ee Bwana, na kwa uaminifu umenitesa.
Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu,
Sawa sawa na ahadi yako kwa mtumishi wako. (K)
Injili. Mk 8: 11-13
Walitokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana na Yesu; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu. Akaugua rohoni mwake, akasema, Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni, Hakitapewa ishara kizazi hiki. Akawaacha akapanda tena chomboni, akaenda zake hata ng’ambo.
TAFAKARI
TUSIMAME IMARA KATIKA MAJARIBU: Majaribu ni fursa ya kutupima uimara na msimamo wa imani yetu. Majaribu katika maisha yetu hayana budi kuja, lakini inatupasa tutumie hekima kubwa kutambua na kuyashinda. Yakobo katika waraka wake kwa kabila kumi na mbili, anawaeleza kuwa wahesabu majaribu kuwa ni furaha tupu, na kujaribiwa kwa imani yao huleta saburi. Saburi ni kukubali mateso, dhiki, na shida kwa ajili ya Mungu. Ni kuwa mvumilivu kwa ahadi za Mungu pasipo kuchoka wala kupoteza imani. Anawasihi wawe na saburi, hekima na waombe dua kwa Mungu, na katika kuomba waombe kwa imani. Namna ya kuwa na saburi inaonekana kwa Yesu ambaye katika utume wake amekuwa akijaribiwa. Yesu hakujibu hovyo, wala hakukata tamaa katika majaribu bali alikuwa mvumilivu na aliendelea na utume wake. Majaribu tuyapatayo katika safari yetu ya kuelekea mbinguni tuyatazame katika jicho la imani. Daima tuwe wavumilivu.
SALA: Tujalie uvumilivu na hekima ya kukabiliana na majaribu Ee Bwana, ili kutokana na uvumilivu wetu tustahilishwe kupata tuzo yetu Mbinguni, amina.