Damu ya Yesu Ipewe Sifa… Karibu Katika Masomo ya Misa 10/02/2024

2024 FEBRUARI 10 JUMAMOSI: JUMA LA 5 LA MWAKAKijani
Zaburi: Juma 1
Mt. Skolastika, Bikira

SOMO 1:  1Fal. 12: 26-32; 13: 33-34

Yeroboamu alisema moyoni mwake:  Basi ufalme utairudia nyumba ya Daudi. Kama watu hawa wakipanda kwenda kutoa dhabihu katika nyumba ya Bwana huko Yerusalemu, ndipo mioyo ya watu hawa itamrudia Bwana wao, yaani, Rehoboamu mfalme wa Yuda; nao wataniua mimi, na kumrudia Rehoboamu, mfalme wa Yuda. Kwa hiyo mfalme akafanya shauri, akafanyiza ng’ombe wawili wa dhahabu, akawaambia watu, Ni vigumu kwenu kupanda kwenda Yerusalemu; tazama, hii ndiyo miungu yenu, enyi Israeli, iliyowapandisha kutoka nchi ya Misri. Akamweka mmoja katika Betheli, na wa pili akamweka katika Dani. Jambo hili likawa dhambi, maana watu walikwenda kuabudu mbele ya kila mmoja, hata huko dani. Tena akafanya nyumba za mahali pa juu akafanya na watu wo wote, watu wasio wa wana wa Lawi, kuwa makuhani. Yeroboamu akaamuru kushika sikukuu katika mwezi wa nane, siku ya kumi na tano ya mwezi, mfano wa sikukuu iliyokuwa katika Yuda, akapanda juu ili kuiendea madhabahu. Akafanya vivyo katika Betheli akiwatolea dhabihu wale ng’ombe aliowafanya; akawaweka katika Betheli wale makuhani wa mahali pa juu alipokuwa amepafanya. Baada ya hayo Yeroboamu hakuiacha njia yake mbovu, lakini akafanya tena makuhani wa mahali pa juu, wa watu wo wote. Kila aliyetaka akamfanya wakfu, ili wawepo makuhani wa mahali pa juu. Jambo hilo likawa dhambi kwa nyumba ya Yeroboamu, hata kuiharibu, na kuifuta usoni pa nchi.

Wimbo wa Katikati. Zab 106: 6-7, 19-22

1. Tumetenda dhambi pamoja na baba zetu,
Tumetenda maovu, tumefanya ubaya.
Baba zetu katika Misri
Hawakufikiri matendo yako ya ajabu. (K)

(K) Ee Bwana, unikumbuke mimi,
      kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.


2. Walifanya ndama huko Horebu,
Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.
Wakaubadili utukufu wao
Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani.

3. Wakamsahau Mungu mwokozi wao,
Aliyetenda makuu katika Misri:
Matendo makuu katika nchi ya Hamu,
Mambo ya kutisha kutisha penye bahari ya Shamu. (K)

Injili. Mk 8: 1-10

Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akawaambia, Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula; nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao hali wanafunga, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali. Wanafunzi wake wakamjibu, Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani? Akawauliza, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba. Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawaandikie, wakawaandikia mkutano. Walikuwa na visamaki vichache; akavibariki, akasema wawaandikie na hivyo pia. Wakala, wakashiba, wakakusanya mabaki ya vipande vya mikate makanda saba. Na watu waliokula wapata elfu nne. Akawaaga. Mara akapanda chomboni pamoja na wanafunzi wake, akaenda pande za Dalmanutha.

Tafakari

WIVU WETU MBAYA HULETA MAPATO MABAYA: Daima tabia ya wivu mbaya hupelekea fikra mbaya, maamuzi mabaya na matokeo yake huwa mabaya. Tunamshuhudia Yerobohamu kwa wivu wake, alifikiri moyoni mwake kwamba ufalme utarudi katika nyumba ya Yuda, Rehoboamu atakuwa mfalme wao na alihofu kuuawa. Kutokana na wivu wake huo aliamua kufanyiza miungu na kuwaambia Waisraeli waiabudu, alifanyiza nyumba na kuwaandaa makuhani kinyume na utaratibu. Wivu wake umepelekea atende dhambi. Wanafunzi wa Yesu ni kinyume kabisa cha Mfalme Yerobohamu, wao walipoulizwa na Yesu juu ya idadi ya mikate waliyokuwa nayo walijibu saba. Wanafunzi hawa hawakuonesha wivu. Yesu mwenyewe hakuona wivu kwa hali yake ya kutenda miujiza, hakuona kuwa mkutano watafaidi, aliwalisha. Wivu mbaya hurudisha maendeleo nyuma, huangamiza, hufifisha imani, hufarakanisha, hunyima haki, ni dhambi. Kuepuka wivu mbaya ni kuepuka dhambi. Hivyo daima tusiwe watu wa wivu.

SALA: Ee Bwana, tunakuomba utujalie moyo wa mapendo na kujali ili tusiangukie katika hali ya wivu mbaya, amina.