Select Page

Kristu Jana… Karibu katika Masomo ya Misa Takatifu 09/02/2024

2024 FEBRUARI 9 IJUMAA: JUMA LA 5 LA MWAKA

Bikira Maria wa Lurdi

Kijani

Zaburi: Juma 1

SOMO 1:  1 Fal. 11: 29-32; 12: 19

Ikawa zamani zile Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao mashambani. Ahiya akalishika lile vazi jipya alilokuwa amelivaa, akalirarua vipande kumi na viwili. Akamwambia Yeroboamu, Twaa wewe vipande kumi, maana Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkono wa Sulemani, nami nitakupa wewe kabila kumi; lakini yeye atakuwa na kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya Yerusalemu, mji ule niliouchagua katika miji yote ya kabila za Israeli. Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi hata leo.

Wimbo wa Katikati. Zab 81:10-15

1. Usiwe na Mungu mgeni ndani yako
Wala usimsujudie mungu mwingine.
Mimi ndimi Bwana Mungu wako
Niliyekupandisha toka nchi ya Misri. (K)

(K) Mimi ndimi Bwana Mungu wako:
         Lisikieni sauti yangu.”

 
2. Watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu,
Wala Israeli hawakunitaka.
Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao,
Waenende katika mashauri yao. (K)

3. Laiti watu wangu wangenisikiliza,
Na Israeli angeenenda katika njia zangu;
Ningewadhili adui zao wa upesi,
Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu. (K)

Injili. Mk 7: 31-37 

Yesu alitoka katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme. 

TAFAKARI

DHAMBI HUNYANG’ANYA UHURU NA MAMLAKA: Tunapokuwa katika hali ya neema na baraka tunakuwa na uhuru na amani katika dhamiri zetu na kwa wale tunaoishi nao, twapata hata fursa ya kuwa viongozi wa maisha yetu na ya wenzetu. Tunapotenda dhambi, tunafifisha na tunaruhusu kuondolewa hali ya kuwa huru na kuongoza. Mfano wa kupoteza mamlaka tunauona kwa Sulemani, kutokana na kosa lake, Taifa linagawanyika na anatwaliwa Yeroboamu kuongoza makabila kumi na Sulemani anaachiwa kabila moja tena kwa heshima ya Daudi na Yerusalemu. Pia Israeli waliasi nyumba ya Daudi. Sulemani anapaswa kumrudia Mungu. kumrudia Mungu kunarejesha ule uzuri alioufanya Mungu wakati wa uumbaji (Mwa 1:31). Ndicho kitendo anachokifanya Yesu kupitia kumponya bubu kiziwi. Mapungufu haya ya bubu kiziwi yanawakilisha mapungufu yetu ubinadamu hasa dhambi. Dhambi zetu zinatukosesha uaminifu, uhuru, amani, nguvu ya kukemea maovu, zinapunguzia utendaji bora. Matokeo yake ni kupoteza nafasi zetu. Hivyo inatupasa tujitahidi kukwepa dhambi ili tujihakikishie uhuru na utendaji bora.

SALA: Twakuomba Ee Bwana utusaidie kutambua na kukiri dhambi zetu ili tuweze kurejesha uhuru na utendaji bora ambao utaleta matunda yafaayo, amina.