Select Page

2024 FEBRUARI 8 ALHAMISI: JUMA LA 5 LA MWAKA

Mt. Skolastika, Bikira

Kumbukumbu

Nyeupe

Zaburi: Juma 1

SOMO 1:  1 Fal. 11: 4-13

Mfalme Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake. Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni, na Milkomu, chukizo la Waamoni. Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake. Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni. Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu. Basi Bwana akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha Bwana, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili, akamwamuru katika habari ya jambo lilo hilo asifuate miungu mingine; lakini yeye hakuyashika aliyoyaamuru Bwana. Kwa hiyo Bwana akamwambia Sulemani, kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitakupa mtumishi wako. Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako. Lakini sitaondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua.

Wimbo wa Katikati.  Zab 106: 3-4, 35-37, 40

1. Heri washikao hukumu,
na kutenda haki siku zote.
Ee Bwana, unikumbuke mimi,
kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako,
unijilie kwa wokovu wako. (K)

(K) Ee Bwana utukumbuke,
       kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.   


2. Walijichanganya na mataifa,
wakajifanyia matendo yao.
Wakazitumikia sanamu zao,
nazo zikawa mtego kwao. (K)

3. Naam walitoa wana wao na binti zao
kwa dhabihu kwa mashetani.
Hasira ya Bwana ikawa juu ya watu wake,
akauchukua urithi wake. (K)

Injili. Mk 7: 24-30 

Yesu aliondoka Nazareti akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba, akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika. Ili mara mwanamke, ambaye binti yake yuna pepo mchafu, alisikia habari zake, akaja akamwangukia miguuni pake. Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake. Akamwambia, waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa. Naye akajibu, akamwambia, naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto. Akamwambia, kwa sababu ya neno hilo, enenda zako; pepo amemtoka binti yako. Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka.   

TAFAKARI

IMANI THABITI KWA MUNGU NI TIBA: Katika imani tunapata nguvu ya kushirikisha changamoto zetu kwa Bwana. Katika Injili tumeshuhudia binti aliyetolewa pepo na Yesu kutokana kitendo cha mama yake kubaki imara katika imani. Yesu anatumia jina mbwa ambalo kwa Wayunani lilibeba dhana ya mbwa mdogo, ambaye Wayunani walimfuga ndani na baada ya watu kula walimrushia mabaki chini ya meza. Jinsi ya kutamka neno hilo mbwa mdogo liliashiria upendo na kujali. Maelezo ya Yesu yaliashiria taifa la Israeli wapate Injili kwanza na wengine wafuatie wakiwemo Wayunani. Yesu anamtoa pepo yule binti kutokana na imani ya mama yake. Namna hii ya kuwa imara katika imani imekuwa kinyume kwa Mfalme Sulemani, kwani ni mara mbili, Bwana Mungu wa Israeli alimuamuru asifuate miungu mingine lakini akapuuza kupitia ushawishi mbaya wa wake zake. Na kutokana na jambo hilo Bwana anaahidi kuurarua ufalme wake. Uhalisia wa kusimama imara katika imani na kutimiziwa haja ndio unapaswa kuwa mwelekeo wetu thabiti mbele ya Mungu. Tumtumainie Mungu daima.

SALA: Mungu, kwa maombezi ya Mt. Skolastika, tunakuomba utusaidie kusimama imara katika imani yetu kwako, amina.