Select Page

Itukuzwe Damu ya Yesu: Karibu Katika Msomo ya Misa 05/02/2024

2024 FEBRUARI 5 JUMATATU: JUMA LA 5 LA MWAKA

Kijani

Zaburi: Juma 1

SOMO 1:  1 Fal.  8: 1-7, 9-13

Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila, wakuu wa mbari za mababa wa wana wa Israeli, wamwendee mfalme Sulemani huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la agano la Bwana kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni. Wakakutana mbele ya mfalme Sulemani watu wote wa Israeli wakati wa sikukuu, katika mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba. Wazee wote wa Israeli wakaja, nao makuhani wakajitwika sanduku. Wakalipandisha sanduku la Bwana, na ile hema ya kukutania, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa katika ile Hema; vitu hivyo makuhani na Walawi wakavipandisha. Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli walikutanika kwake, walikuwako pamoja naye mbele ya sanduku, wakichinja sadaka kondoo na ng’ombe, wasioweza kuhesabiwa wala kufahamiwa idadi yao kwa kuwa wengi. Makuhani wakalileta sanduku la agano la Bwana hata mahali pake, katika chumba cha ndani cha ile nyumba, patakatifu pa patakatifu, naam, chini ya mbawa za makerubi. Kwa maana makerubi yalinyosha mbawa zao juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu.  Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, Bwana alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri. Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya Bwana ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya Bwana ilikuwa imejaa utukufu wa Bwana. Ndipo Sulemani akanena, Bwana alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele.

Wimbo wa Katikati. Zab 132: 6-10

1. Tazama, tulisikia habari zake katika Efrata,
katika konde Yearimu tuliiona.
Na tuingie katika maskani yake,
tusujudu penye kiti cha kuwekea miguu yake. (K)

(K) Ee Bwana, uinuke, uende kwenye raha yako.

2. Ee Bwana, uinuke, uende kwenye raha yako,
Wewe na sanduku la nguvu zako.
Makuhani wako na wavikwe haki,
watauwa wako na washangilie.
Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako,
usiurudishe nyuma uso wa masihi wako. (K)

Injili. Mk 6: 53-56 

Yesu na wanafunzi wake walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. Nao wakiisha kutoka mashuani, mara watu walimtambua, wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi, kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo. Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona.

TAFAKARI

NGUVU YA MUNGU INAPONYA: Nguvu ya Mungu inawezesha mambo yote hata kuponya mwili na roho. Nguvu ya Mungu inahitaji imani yetu kwake. Nguvu ya Mungu imewaponya wagonjwa kwa kugusa pindo la vazi la Yesu. Wagonjwa walimsihi Yesu waguse pindo la vazi lake kwasababu waliamini juu ya nguvu ya uponyaji iliyo ndani yake. Pia, Nguvu hii ya Mungu inatambuliwa na Waisraeli katika kulifuata agano lao na Mungu. Utambuzi huu ndio uliomsukuma Mfalme Sulemani kuwaita Waisraeli ili walipandishe Sanduku la Agano kutoka mji wa Daudi, mji wa Sayuni. Walipolipandisha walifurahi, na utukufu wa Mungu ulijaa ndani ya nyumba. Utukufu huu ndiyo nguvu ya Mungu iliyodhihirika mbele ya Waisraeli. Wapendwa, katika maisha yetu, magumu tunayokutana nayo tuyapeleke mbele ya Mungu. Daima tuwe watu wenye imani kwamba Mungu ndiye mwenye kutupa ufumbuzi wa changamoto katika maisha yetu. Tuliguse pindo la vazi la Yesu kwa kufuata na kuzii Amri za Mungu, kwa kuishi amri Kuu ya Mapendo. Nguvu za Mungu zinatuponya, tuzikimbilie.

SALA: Ee Mungu tujalie daima tutambue nguvu zako na kwa njia ya imani kwako tuweze kupata ahueni ya maisha yetu, amina.