Select Page

Damu ya Yesu Itukuzwe. Karibu Katika masomo ya Misa Takatifu.

2024 FEBRUARI 1 JUMAPILI: DOMINIKA YA 5 YA MWAKA

Kijani

Zaburi: Juma 1

Somo 1. Ayu 7:1- 4, 6-7

Ayubu alianza kusema: Je! Mtu hana wakati wake wa vita juu ya nchi?  Na siku zake, je! si kama siku za mwajiriwa? Kama mtumishi atamaniye sana kile kivuli, kama mwajiriwa anayetazamia mshahara wake; ni vivyo nami nimepewa miezi ya ubatili iwe fungu langu, Nami mimeandikiwa masiku yenye kuchokesha. Hapo nilalapo chini, nasema, Nitaondoka lini? lakini usiku huwa mrefu; Nami nimejawa na kujitupa huku na huku hata kupambazuke. Siku zangu hupita upesi kuliko chombo cha kufumia, Nazo zapita pasipokuwa na matumaini. Kumbuka ya kwamba maisha yangu ni upepo; Jicho langu halitaona mema tena.

Wimbo wa Katikati. Zab 147: 1-6

1. Aleluya.
Msifuni Bwana;
Maana ni vema kumwimbia Mungu wetu,
Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri. (K)

(K) Msifuni Bwana, huwaponya waliopondeka moyo.

2. Bwana ndiye aijengaye Yerusalemu,
Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli.
Huwaponya waliopondeka moyo,
Na kuziganga jeraha zao.
Huihesabu idadi za nyota 
Huzipa zote majina. (K)

3. Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu,
Akili zake hazina mpaka.
Bwana huwategemeza wenye upole,
Huwaangusha chini wenye jeuri. (K)

Somo 2. 1 Kor 9: 16 -19, 22 – 23

Ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili! Maana nikiitenda kazi hii kwa hiyari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiyari yangu, nimeaminiwa uwakili. Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo, nitaitoa Injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili. Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi. Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu. Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine.

Injili. Mk 1: 29-39

Walipotoka katika sinagogi, Yesu pamoja na Yakobo na Yohane, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo. Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua. Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko. Simoni na wenziwe wakamfuata; nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta. Akawaambia, Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hilo nalitokea. Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo.

TAFAKARI

MATESO NA TAABU ULIMWENGUNI NI ZAO LA UASI WA MWANADAMU; PALIPO NA MUNGU FURAHA YA NDANI HUTAWALA
Tungo moja ya nyimbo za dini inakwenda namna hii: “Nikitazama juu angani nikiomba msaada, mateso yananizidi, hakuna anayekuja, nainua mikono yangu naleta sala yangu, Ee Mungu nisaidie, Mungu unihurumie.” Ni tungo inayotupatia taswira ya mwanadamu aliye kwa upande mmoja katika hali ya mateso na kwa upande mwingine inamwonesha akiweka tegemeo lake kwa Mungu. Shida, mahangaiko na taabu huandamana na maisha ya kila siku ya mwanadamu. Wengine huimarishwa katika imani yao lakini wengine huweweseka na kuiacha imani. Pamoja na hayo yote tunapaswa kujiuliza chanzo chake ni nini? Kama Mungu aliumba vyote na akasema kuwa ni vizuri wapi yanapotokea haya? Ninawaalika katika Dominika hii kutafakari juu ya dhana hii.
Tuanze kwa kujiuliza: Je, ipo wapi imani yangu na utegemezi wangu kwa Mungu pale ninapokumbwa na matatizo fulani? Je, ninapokimbilia kwa nguvu nyingine na kumwacha Mungu ni suluisho kwa shida ninazozipata? Je, matatizo niliyonayo yamesababishwa na yeye? Maandiko matakatifu yatuonesha wazi ni wapi unapotokea uovu dhidi ya mwanadamu; si kutoka kwa mwenyezi Mungu bali ni husuda na nia mbaya ya mwovu shetani. Ibilisi ndiye alimpatia Ayubu maswahibu yaliyompata (rej. Ayu 1:9-12). Hivyo chanzo cha uovu hakiwezi kutoka kwa Mungu. Hata katika jamii ya mwanadamu leo hii tunaona hivyo. Ni husuda, wivu, majigambo na chuki za kibinadamu ndizo ambazo zinauharibu ulimwengu huu na kumfanya mwanadamu daima kuwa katika hali ya mahangaiko. Katika ujumla wake tunaweza kuona hali hii katika tendo la mwanadamu kumweka pembeni Mungu na kujitwalia utawala wake binafsi, jambo ambalo linazaa ubinafsi na kuua undugu kati ya watu.
Simulizi la Ayubu katika somo la kwanza ni kielelezo kwetu na jawabu kwa mwitikio wetu wakati wa kukabiliana na maswahibu katika maisha. Imani yake kwa Mungu haiyumbishwi na haya yanayompata. Daima anauona wema wa Mungu na anayachukulia hayo yanayomsibu kuwa hayatoki kwake na mwishoni yatapita na yeye kuendelea kuuonja wema wa Mungu. Anaonesha wazi kwamba mwanadamu kupitia katika maswahibu ni jambo la kawaida na wakati mwingine linakatisha tamaa. Hali hii haimuondoi katika kuweka tumaini lake kwa Mungu. Ayubu aliyekirimiwa mali nyingi na umaarufu mkubwa alipitia katika wakati mgumu sana. Ni kipindi cha majaribu ambacho kilinuia kuipima imani yake. Wote waliomzunguka walidiriki hata kumshawishi amtukane Mungu. Lakini yeye aliyaangalia yote katika jicho la imani na kuungana na mzaburi na kutualika akisema: “Msifuni Bwana, huwaponya waliopondeka moyo.” Anakuwa mithili ya Kristo pale juu msalabani katika hali ya mateso makubwa alijikabidhisha kwa Mungu akisema: “Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu” (Lk 23:46).
Uasi wa mwanadamu ulimwondoa Mungu katikati ya watu na kuwa chanzo cha mivurugano na taabu nyingi. Uasi huu uliiharibu kazi ya uumbaji na kumfanya mwanadamu kupitia katika hali ya shida. Ujio wa Kristo ulimwenguni unahuisha tena uwepo wa Mungu na hivyo kuwa sababu ya furaha na auheni kwa mwanadamu. Hili linajidhihirisha katika somo la Injili ya leo pale Kristo anapowaponya watu mbalimbali walioletwa mbele yake kwa ajili ya uponyaji. Mama mkwe wa Petro ni mmoja kati ya hawa wanaoponywa na tunaambiwa baada ya kupokea uponyaji “homa ikamwacha, akawatumikia.” Tendo hili linatufundisha jambo muhimu sana juu ya nini kinacholetwa na Kristo na matokeo yanayotegemewa kutoka kwetu sisi. Mama mkwe wa Petro na hawa wengine wanaoponywa wanauwakilisha ubinadamu unaogaragazwa na taabu za ulimwengu huu. Ujio wa Kristo ambao ni utambulisho wa uwepo wa Mungu unaleta uponyaji. Ujio wa Kristo ulimwenguni ulinuia kumkomboa mwanadamu. Uumbaji wote ambao umekuwa katika hali ya kuvurugika umerudishwa katika uwiano.
Zaidi ya hapo ujio wake unafanya uumbaji uendelee katika hali yake njema. Mama mkwe wa Petro alipoponywa aliwahudumia. Alirudi katika nafasi yake ya kawaida kama mama na kuwahudumia. Bila shaka kabla ya kuponywa wageni waliofika wakisongwa na uchovu na njaa kidogo walipoteza matumaini na pia kuugua pamoja naye. Hii ndiyo hali ya ulimwengu wetu pale ambapo bado haujaonja uwepo wa Mungu. Ni mahali ambapo panabaki kutokuwa na matumaini na furaha kwa wenye uhitaji. Uwepo wa Mungu hurejesha furaha na kutoa fursa kwa kila mwanajamii na kila kiumbe kutimiza wajibu wake sawasawa na katika hali hiyo kila mmoja kuwa faida kwa mwenzake. Haya ni matibabu kwa jamii ya mwanadamu inayogawanyika na inayomwachia kila mmoja ajitafutie auheni yake mwenyewe na matokeo yake ni magovi, chuki na husuda ambazo kuendelea kumwacha mwanadamu mateso maishani mwake.
Ujio wa Kristo ni uumbaji mpya. Ujio huu mpya unatufanya kuwa wapya na pia kutuweka kuwa vyombo vya kuieneza habari hii njema kwa wote. Hayo tuyaonjayo kwa ujio wake na mwanzo huu mpya hutusukuma kuwashirikisha na wengine ili kwa huduma zetu nao wauone mkono wa Mungu. Mtume Paulo anayekutana na uponyaji wa ndani baada ya kukutana na Kristo (rejea tukio la njiani kuelekea Dameski (rej. Mdo 9:3-6) anabadilika na kuichangamkia kazi ya kumhubiri Kristo. Yeye anasema waziwazi kwamba: “Ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili.” Yeye ambaye alikuwa mwanzo mpinzani wa Injili, alikuwa bado mgonjwa kiroho kwa kutokukutana na Kristo aliye uzima wa wanadamu, sasa anapata uponyaji na kugeuka kuwa mhubiri maarufu na mtetezi wa Injili. Anakutana na Kristo, anampatia uponyaji, anajaa furaha na mara moja anaanza kuwahudumia ndugu zake. Paulo anatuhasa kutumia fursa tuipatayo ndani ya Kristo, yaani uzima wa kimungu unaorejeshwa ndani mwetu kwa kujitoa na kutenda kwa busara ili kuwafikia wote katika hali zote. Hii ni kuwa mithili ya Kristo ambaye ameitwaa hali yetu ya kibinadamu ili apate kutukomboa. Mwenyezi Mungu anakutuma kwenda kuitangaza hari njema na kumrejeshea mwanadamu atesekaye matumaini huku ukimwendea kwa hali yake, lugha yake na namna yake na hivyo kukuelewa vizuri.
Mkristo ni kiumbe mpya. Sakramenti ya ubatizo inampatia cheo hicho na kwa Sakramenti ya Ekaristi takatifu anaungana kwa karibu zaidi na upendo wa Mungu na hivyo anatarajiwa kutoa miale upendo huo na kuangaza kote. Wapo wanadamu ambao bado wanateseka lakini hawajapoteza matumaini kwa Mungu; wapo ambao ni wagonjwa, wapo waliopoteza wapendwa wao, wapo waliopoteza mali zao. Wote wanamlilia Mungu na wanategemea uponyaji wa ndani. Tunapaswa sisi kuwa vyombo vya kuwarudishia matumaini na kuyapokea yote katika imani. Tutende hayo kwa maneno yetu na mfano wa maisha yetu yanayoakisi ukweli wa injili kwani Kristo aliye Injili yetu “aliutwaa udhaifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu.”