Atukuzwe Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa 03/02/2024
2024 FEBRUARI 3 JUMAMOSI: JUMA LA 4 LA MWAKA
Mt. Hieronimo Emiliano
Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: 1 Fal. 3: 4-13
Mfalme Sulemani alienda Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu ya madhabahu ile. Na huko Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani akasema, “Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?” Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili. Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu; basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe. Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote.”
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 119: 9-14
Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii akilifuata neno lako. Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, usiniache nipotee mbani na maagizo yako.
(K) Unifundishe amri zako, Ee Bwana.
Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi. Ee Bwana umehimidiwa, unifundishe amri zako. (K)
Kwa midomo yangu nimezisimulia hukumu zote za kinywa chako. Nimefurahi njia ya shuhuda zako kana kwamba ni mali mengi. (K)
INJILI: Mk. 6:30-34
Mitume walikusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha. Akawaambia, “Njoni ninyi peke yenu kwa faragha; mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo.” Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu. Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika. Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi.
TAFAKARI
HEKIMA NI DIRA BORA KATIKA KUONGOZA: Katika kuomba kwake kwa Bwana, Mfalme Sulemani aliomba moyo wa adili ili awahukumu kwa haki na aweze kupambanua mema na mabaya. Mfalme Sulemani hakutaka maisha bora wala namna ya kuwazidi adui zake. Bwana anapendezwa na ombi lake na anampa moyo wa hekima na wa akili, pia akampa hata yale ambayo hakuomba. Katika Injili tunaona muendelezo wa wazo la hekima linalodhihirishwa na Mitume wa Yesu, ambao kwa hekima yao wanapeleka mrejesho kwa Yesu juu ya utume waliopewa naye. Yesu kwa kutambua hekima yao anawaita faragha ili wapumzike. Pia kutokana na hekima yao katika utume ilipelekea watu wengi kuwafuata na Yesu alipowaona kama kondoo wasio na mchungaji aliwafundisha. Tutambue kuwa hekima imekuwa dira bora kwa Sulemani, kwa Mitume hata kwa Kristo mwenyewe. Katika ukristo wetu, tunapaswa kuwa dira kwa wenzetu, kwa maisha yetu bora tunakuwa viongozi, hivyo daima tunapaswa kuenenda vema. Huku ndiko kuwa na hekima iliyo zawadi kutoka kwa Mungu.
SALA: Ee Bwana tujalie hekima na busara ili tunapofanya maamuzi katika maisha yetu na ya wenzetu tuamue vema, amina.