Select Page

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa 02/02/2024

2024 FEBRUARI 2 IJUMAA:

KUTOLEWA BWANA HEKALUNI                                                                                                                                           

Sikukuu

Nyeupe

Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1:  Mal.  3:1-4

Bwana Mungu asema hivi: Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni  mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo: naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.

WIMBO WA KATIKATI:                Zab. 24:7-10

Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Inukeni, enyi malango ya milele.

(K) Ni nani mfalme wa utukufu?

Ni Bwana, mwenye nguvu, hodari. Ni nani Mfalme wa utukufu? Bwana mwenye nguvu, hodari, Bwana hodari wa vita. (K)

Inueni vichwa vyenu, enyi milango, Naam, viinueni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia. (K)

Ni nani huyu Mfalme wa utukufu? Bwana wa majeshi, Yeye ndiye Mfalme wa utukufu. (K)

  •             

SOMO 2:  Ebr. 2:14-18

Kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa. Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.

SHANGILIO       Lk. 2:32

Aleluya, aleluya

Nuru ya kuwa mwangaza wa mataifa,

na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.

Aleluya.

INJILI:  Lk. 2:22-40

Zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa, wazee wa Yesu walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana, wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mkononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, “Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, kwa amani, kama ulivyosema; kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, uliouweka tayari machoni pa watu wote; nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.” Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, “Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.” Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya, mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

“Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mkononi mwake

TAFAKARI

UKRISTO NI SADAKA KWA AJILI YA KAZI YA MUNGU: Leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni. Sikukuu hii itukumbushe juu ya Sakramenti ya ubatizo na ahadi zake. Katika Ubatizo tunatolewa na kujitoa rasmi kwaajili ya utume wa Kristo, tunatolewa kuwa wafuasi wake Kristo. Zilipotimia sikukuu za kutakasika kwao, wazazi wa Yesu nao walikwenda kumtolea mbele za Mungu. Kutolewa Bwana Hekaluni kunadhihirisha upekee wa utume wa Kristo katika kutekeleza kazi ya kutukomboa wanadamu. Maisha yake Yesu yanarasimishwa, yanatengwa, yanatolewa ili kutimiza mpango wa Mungu katika kutukomboa wanadamu. Bwana anayetolewa hekaluni ndiye mjumbe wa Agano aliyefurahiwa. Huyu ndiye anayetajwa na nabii Malaki katika somo la kwanza. Tunaalikwa kujua na kutazamia hali zetu pindi atakapokuja. Ndugu zangu, tunapompokea Kristo aliyetolewa hekaluni, tunaupokea Ukristo wetu na kuukili kuwa ndio njia ya kuupata utakatifu, hivyo inatupasa kujiandaa.

SALA: Ee Mwenyezi Mungu, utujalie katika ukristo wetu kujitoa na kujitolea ili kazi ya ukombozi wetu iweze kuendelea, amina.