Select Page

Kristu Jana. Karibu Katika Masomo ya Misa 01/02/2024

2024 FEBRUARI 1  ALHAMISI: JUMA LA 4 LA MWAKA

Wat. Paulo Miki na Wenzake, Mashahidi

Kumbukumbu

Kijani

Zaburi: Juma 4

SOMO 1:  1 Fal 2: 1-4, 10-12

Siku ya kufa kwake Daudi ilikaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, “Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mahusia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako; ili Bwana afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu, akisema, ‘Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema,) hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha Israeli.’”  Basi Daudi akalala na babaze, akazikwa mjini mwa Daudi. Na siku alizotawala Daudi juu ya Israeli zilikuwa miaka arobaini; huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelethini na mitatu.  Basi Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Daudi baba yake; na ufalme wake ukawa imara sana.

WIMBO WA KATIKATI:               Nya.  29: 10- 12

Uhimidiwe, ee Bwana, Mungu wa Israeli baba yetu milele na milele.

(K) Nawe watawala juu ya vyote, Ee Bwana.        

Ee Bwana, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako. (K)

Ufalme ni wako, Ee Bwana, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe. (K)

Nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. (K)

INJILI:  Mk. 6:7-13

Siku ile Yesu aliwaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; lakini wajifungie viatu, akasema, “Msivae kanzu mbili.” Akawaambia, “Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale. Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung’uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao.” Wakatoka, wakahuburi kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.

TAFAKARI

UTII NI BORA KULIKO SADAKA: Mfalme Sulemani (Mwana wa Daudi) alipotawala, ufalme wake ulikuwa imara sana kwasababu alitii na kufuata wosia wa baba yake. Mafanikio ya namna hiyo yanashuhudiwa na Thenashara ambao walihubiri juu ya toba, na walifanikiwa kutoa pepo wengi, waliwapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa na waliwapoza. Walifanikiwa kwasababu walifuata maelekezo waliyopewa na Yesu. Wapendwa katika Kristo, katika Ukristo wetu tuna makatazo mbalimbali, tuna amri za Mungu, za Kanisa, na  miiko mbalimbali. Pia katika jamii zetu tuna makatazo mbalimbali. Makatazo yenye kumtukuza na kumsifu Mungu ni vema yakafuatwa. Tunapopuuza tunaupuuza wokovu wetu. Tukumbuke kuwa, “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu” pia “Aisifiaye mvua imemnyea”. Wapendwa, kuvunja makatazo ni kukubali kubaki katika hali ya dhambi. Tukiisifu dhambi itatufanya tuwe watumwa daima na mwisho  itatukosesha Utukufu wa Mungu.

SALA: Ee Baba, tunakuomba daima utujalie neema ya kufuata maagizo ili tuweze kuurithi Ufalme wako, amina.