Masomo ya Misa Januari 31

Damu ya Yesu Ipewe Sifa. Karibu Katika Masomo ya Misa 31/01/2024

2024 JANUARI 31 JUMATANO: JUMA LA 4 LA MWAKA

 Mt. Agata, Bikira na Shahidi

Kumbukumbu

Kijani

Zaburi: Juma 4


SOMO 1:  2 Sam. 24: 2, 9-17

Mfalme Daudi alimwambia Yoabu, jemadari wa jeshi la askari, waliokuwa pamoja naye, “Zunguka sasa katikati ya kabila zote za Israeli, tangu Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu, nipate kujua jumla ya hao watu.” Naye Yoabu akamtolea mfalme jumla ya hesabu ya watu; nao walikuwa wa Israeli mashujaa wenye kufuta panga mia nane elfu; nao wa Yuda walikuwa watu mia tano elfu.  Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia Bwana, “Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee Bwana, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.” Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la Bwana likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, kusema, “Nenda, ukanene na Daudi, Bwana asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo.”  Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza akamwambia, “Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.” Naye Daudi akamwambia Gadi, “nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa Bwana; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.”  Basi Bwana akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hata wakati ulioamriwa; nao wakafa watu toka Dani mpaka Beer-sheba sabini elfu. Lakini huyo malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili auharibu, Bwana akaghairi katika mabaya, akamwambia huyo malaika mwenye kuwaharibu watu, “Yatosha, sasa ulegeze mkono wako.” Naye yule malaika wa Bwana alikuwako karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi. Daudi, alipomwona malaika aliyewapiga watu, akanena na Bwana, akasema, “tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu!”

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 32: 1-2, 5-7

Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake. Heri Bwana asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni mwake hamna hila. (K)

(K) Ee Bwana,  unisamehe upotovu wa dhambi yangu.

Nalikujulisha dhambi yangu, Wala sikuuficha upotovu wangu. (K)

    INJILI:  Mk. 6:1-6

    Yesu alitoka huko, akafika mpaka nchi ya kwao, wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, “Huyu ameyapata wapi haya?” na, “Ni hekima gani hii aliyopewa huyu?” na, “Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? na maumbu yake hawapo hapa petu?” Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake.” Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko; isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya. Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao.


    TAFAKARI

    UNYENYEKEVU NI HEKIMA YA KIMUNGU: Unyenyekevu ni hali ya kujishusha, hali ya kujiweka kawaida, ya kutambua na kuthamini kuwa tulivyonavyo si kwa mastahili yetu ila ni kwa mpango wa Mungu. Yesu Kristo aliishi maisha ya kujishusha, maisha ya kawaida licha ya upekee wake. Hali hii ya maisha yake ndiyo iliyopelekea watu wastaajabie hekima aliyokuwa nayo kwani aliwafundisha watu wa kwao ambao waliyafahamu maisha yake ya kawaida. Namna nyingine ya kujishusha tunashuhudiwa pia na Daudi ambaye anatambua kuwa yeye ndiye aliyekosa na anastahili adhabu, si wengine. Hekima ya Daudi ndiyo inamfanya atambue kuwa amekosa na anastahili adhabu. Ndugu zangu katika Kristo, hekima yetu hutokana na kutojikweza, kutojiona wa pekee hasa kwa jamii tulizotoka na zilizotukuza. Kwa kuwa na hekima tunakuwa walimu kwa wenzetu, kile kinachofundishwa kwa kuwa ni zao la hekima ya kimungu kitawasaidia watu na wataona mchango wake. Pia tunapokuwa na hekima tunatambua kuwa sisi tu wadhaifu hivyo inatupa nafasi ya kujitathmini na kufanya mabadiliko.

    SALA: Ee Mungu, tunakuomba utujalie hekima ili tunapoamua na kutenda tutende kadiri ya mpango wako na daima, maamuzi yetu thabiti yawe fundisho kwa wengine, amina.

    About the Author

    One thought on “Masomo ya Misa Januari 31

    Leave a Reply

    Your email address will not be published. Required fields are marked *

    You may also like these