Select Page

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 29/01/2024

2024 JANUARI 29 JUMATATU: JUMA LA 4 LA MWAKA

Mt. Yohane Bosko, Padre

Kumbukumbu

Nyeupe

Zaburi: Juma 4

SOMO 1:  2 Sam. 15: 13-14. 30; 16: 5-13

Mjumbe alimfikilia Daudi, akasema, Mioyo ya watu wa Israeli inashikamana na Absalomu. Basi Daudi akawaambia watumishi wake wote waliokuwa pamoja naye Yerusalemu, Ondokeni, tukakimbie; kwa kuwa tusipokimbia hapana mtu miongoni mwenu atakayeokoka mikononi mwa Absalomu; haya! fanyeni haraka, tuondoke, asitupate kwa upesi, na kutuletea maovu, na kuupiga mji huu kwa makali ya upanga.  Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake; akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda.  Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda. Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto. Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa! Bwana amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli, ambaye umetawala badala yake; naye Bwana ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu.   Ndipo Abishai, mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake. Mfalme akasema, nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu Bwana amemwambia, mlaani Daudi; basi, ni nani atakayesema, mbona umetenda haya? Daudi akamwambia Abishai na watumishi wake wote, angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza. Labda Bwana atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye Bwana atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo. Basi wakaendelea njiani Daudi na watu wake.

WIMBO WA KATIKATI:              Zab. 3: 1-7

Bwana, watesi wangu wamezidi kuwa wengi, Ni wengi wanaonishambilia, Ni wengi wanaoiambia nafsi yangu: Hana wokovu huyu kwa Mungu.

K: Bwana, uinuke, uniokoe.

Na Wewe, Bwana, u ngao yangu pande zote, Utukufu wangu na mwinua kichwa changu. Kwa sauti yangu namwita Bwana, Naye aniitikia toka mlima wake mtakatifu. (K)

Nalijilaza nikalala usingizi, nikaamka kwa kuwa Bwana ananitegemeza. Sitaogopa makumi elfu ya watu Waliojipanga juu yangu pande zote.Bwana, uinuke, Mungu wangu, uniokoe. (K)

INJILI:  Mk.  5:1-20

Yesu na wanafunzi wake walifika ng`ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi. Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo; kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda.  Na siku zote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe.

Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu?  Nakuapisha kwa Mungu usinitese. Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu.  Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi.  Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile.  Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha.  Pepo wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao.  Akawapa ruhusa.  Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini. Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashamba. Watu wakatoka walione lililotokea. Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi; wakaogopa. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza ni mambo gani yaliyompata yule mwenye pepo, na habari za nguruwe. Wakaanza kumsihi aondoke mipakani mwao. Naye alipokuwa akipanda chomboni, yule aliyekuwa na pepo akamsihi kwamba awe pamoja naye; lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu.  Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu.

TAFAKARI

NENA BWANA NAMI NITATII: Yesu Kristo awaamuru pepo wachafu wamtoke mtu waliyempagawa, nao wanamtii kwa kumuacha na kuwaingia nguruwe. Pia Yesu anamwambia aliyekuwa na pepo aende nyumbani kwake, kwa watu wa kwao, akawahubiri mambo makuu aliyotendewa na Bwana. Naye anatii na kwenda kuhubiri katika Dekapoli. Pepo wachafu walimtii Yesu kwa kumuacha mtu waliyemwingia wakaenda kuwaingia nguruwe. Namna hii ya kutii tunashuhudiwa na Daudi aliyemtii Bwana ambaye alimwagiza Shimei amlaani kutokana na uovu wake. Daudi anamkataza Abishai na wenzake wasimwangamize Shimei, anawaambia wamwache kwasababu Bwana ndiye aliyemwagiza. Daudi alitumaini kuwa Bwana atamlipa mema. Wapendwa, katika maisha utii unatupatia ahueni ya maisha yetu, tunapotii tunapata kile tunachostahili. Mapenzi yetu yanatimizwa kadiri ya namna tunavyotii kwa wale wanaopaswa kututimizia. Tena tukumbuke kuwa “utii ni bora kuliko sadaka”

SALA: Ee Mungu utujalie hali ya utii katika maisha yetu ili tuweze kutekeleza na kutimiza wajibu wetu ifaavyo kadiri ya maagizo, amina.