Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa 28/01/2024
2024 JANUARI 28 JUMAPILI: FOURTH SUNDAY IN ORDINARY TIME
Zaburi: Juma 4
Kijani
Somo 1 Kum 18:15-20
Bwana, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye. Kama vile ulivyotaka kwa Bwana, Mungu wako, huko Horebu, siku ya kusanyiko, ukisema, nisisikie tena sauti ya Bwana, Mungu wangu, wala nisiuone tena moto huu mkubwa, nisije nikafa. Bwana akaniambia, wametenda vema kusema walivyosema. Mimi nitawaondoshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru. Hata itakuwa, mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake. Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa.
Wimbo wa Katikati Zab 95:1-2, 6-9.
(K) Ingekuwa Heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu.
1. Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)
2. Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo wa mkono wake. (K)
3. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba,
Kama siku ya Masa jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)
Somo 2 1 Kor 7: 32-35
Wapendwa, nataka msiwe na masumbufu. Yeye asiyeoa hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendezeje Bwana; bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe. Tena iko tofauti hii kati ya mke na mwanamwali. Yeye asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana, apate kuwa mtakatifu mwili na roho. Lakini yeye aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mumewe. Nasema hayo niwafaidie; si kwamba niwategee tanzi, bali kwa ajili ya vile vipendezavyo, tena mpate kumhudumia Bwana pasipokuvutwa na mambo mengine.
Injili Mk 1: 21-28
Yesu alishika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi. Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakaifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema. Nini hii? Ni elimu mpya! maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya.
TAFAKARI
UWEZO WA MUNGU UNAFUNULIWA KATIKA NAFSI YA KRISTO
Moja ya jukumu tunalopewa na Mama Kanisa ni kutangaza neno la Mungu kwa watu wote. Huu ni wajibu wa kinabii ambao unatufanya kila mbatizwa kuwa chombo cha kuwatangazia watu wengine, waliokwisha kulisikia neno na wale ambao bado hawajalisikia ukweli ambao wanafunuliwa na Mungu. Ni wajibu ambao unahitaji utulivu ili kulisikia neno lenyewe na utayari wa kutoka na kuwaambia waliokusudiwa ujumbe uliotumwa. Nabii anatumika kama sauti, kile anachokitangaza si kutoka kwake bali ni kutoka kwa Mungu anayemtuma. Neno la Mungu ambalo nabii hutumwa kulitangaza linanuia kutambulisha uwezo na Mungu katika jamii ya mwanadamu na hivyo kuwezesha yote kufanyika kadiri ya mapenzi ya Mungu.
Dominika ya nne ya Mwaka inatufafanulia dhana hii ya unabii. Katika somo la kwanza tunaona jinsi ambavyo manabii walivyochipuka katika jamii ya Waisraeli. Wana wa Israeli huko Horebu waliomba wapewe nabii kusudi wasimsikilize Mungu moja kwa moja. Mwenyezi Mungu aliwajibu kwa kusema: “mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao… nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.” Hapa tunaona mantiki ya kuwa na nabii katikati yetu. Yeye anakuwa ni mtu tunayeishi naye na tunafahamiana naye vizuri kabisa. Zaidi ya hayo anayafahamu vema mazingira yetu na changamoto zake. Kupitia kwake mwenyezi Mungu anafikisha ujumbe wake na akitegemea utafika katika namna iliyozoeleka na itakayoeleweka. Hivyo tunaweza kuona dhana ya unabii ni mithili ya utamadunisho, ambapo makusudio ya Mungu yanafikishwa mahali mahsusi katika muktadha ulizoeleka na wote na kwa namna hiyo unategemewa kueleweka na kupokelewa vizuri.
Sehemu hiyo ya somo la kwanza inatufafanulia kuwa ujumbe na maudhui ya unabii ni kutoka kwa Mungu mwenyewe. Neno la Mungu linasema: “nami nitatia maneno yangu kinywani mwake.” Kutokusikiliza ujumbe huo utatugharimu lakini pia kama nabii ataelezea maneno yake kwa ajili ya manufaa yake mwenyewe naye pia ataadhibiwa. Ni msisitizo wa kuheshimu maelekezo ya ujumbe wa neno la Mungu. Hapa tunatahadharishwa kuepuka vishawishi vya aina yoyote ambavyo vinaweza kutuhadaa na kulipa kisogo neno la Mungu au wakati mwingine kutafuta njia za kulipindisha au kulichakachua neno la Mungu. Pengine ni hamu ya kutaka kuendeleza sifa za kidunia au kukuza jina lako au kudhulumu jirani yako na pindi neno la Mungu linapokukumbusha wajibu wako unatoa mwitikio hasi. Hapo utakuta mmoja anashindwa kulitangaza kikamilifu kama nabii au anashindwa kulipokea na kulifanyia kazi neno la nabii.
Kristo ambaye ndiye Neno lenyewe la Mungu. Yeye, Neno anayemwilika anaonekana moja kwa moja kwa matendo yake, na uwepo wake unaifanya hadhira yake kuuona mkono wa Mungu. Watu “walimshangaa sana kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa anafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi.” Unabii wake unadhihirika katika nafsi yake na matendo yake hayawi ya kinafki kama ya waandishi na wakuu wa dini wa wakati wake. Mafarisayo na waandishi walijikinai kutoa ujumbe wa neno la Mungu ili hali wao wenyewe hawakuwa wanautimiza. Unabii wao ulikuwa si kulifunua neno la Mungu bali kujitukuza wao wenyewe. Neno la Kristo ni ukweli kwa sababu yeye mwenyewe ndiyo huo kweli yenyewe. Yeye anaufunua uwezo wa Mungu na hivyo anakuwa ni mwiba kwa ibilisi na mawakala wake. Ujio wake kati yetu unafukuza giza la dhambi na mauti.
Katika ubatizo wetu tunapokea wajibu wa kinabii. Kwa Sakramenti hii tunafanywa kuwa wana warithi wa Mungu na kuwa ndugu zake Kristo. Kwa maneno mengine uweza wa Kristo unadhihirika ndani mwetu. Hivyo, uwepo wa wakristo duniani unapaswa kuwa ni mwiba kwa uovu wa ulimwengu huu. Uovu unapoendelea kutamalaki ni mashtaka kwetu kwamba tumeshindwa kuwa neno la Mungu na uwepo wetu hauzitetemeshi nguvu za mwovu. Hii inatokea pale tunapoisahau hadhi yetu na kujisawazisha na ulimwengu huu. Daima tutambue kwamba, hadhi yetu ya kikristo inapaswa kuhuishwa mara kwa mara kwa muunganiko wa kudumu na Mungu. Maisha yetu ya kiroho ndiyo nyenzo pekee ya kuufanya hai uwepo wa Kristo ndani mwetu na hivyo kutufanya kuwa vyombo vya kulieneza neno la Mungu na tishio kwa uwepo wa nguvu za giza.
Mtume Paulo anatuwekea mazingira mbalimbali ya miito yetu ambayo kila mmoja anapaswa kuicheza vyema nafasi yake kwa ajili ya kutekeleza kikamilifu kazi ya kinabii. Mmoja katika maisha ya ndoa anakuwa nabii pale tu anapotimiza wajibu wake kama anavyotegemewa ndani ya ndoa. Kwao wote msisitizo wa kufanya yote kikamilifu kwa ajili ya furaha ya kweli ya mwenzi wake. Kwa upande wao wanaojiweka katika maisha ya wakfu wanakumbushwa kutekeleza kwa ajili ya Bwana. Paulo anahitimisha kwa kusema: “Nasema hayo niwafaidie; si kwamba niwategee tanzi, bali kwa ajili ya vile vipendezavyo, tena mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine.” Ni wito ambao unaturudisha katika wazo moja tunalotafakari leo hii kwamba: yote yanapaswa kufanyika kwa ajili ya kudhihirisha ukuu wa Mungu.
Kristo anatufunulia ukuu wa Mungu katika nafsi yake. Sisi tulio wajumbe wake tunaalikwa kutimiza nyajibu zetu mbalimbali kiaminifu ili kazi zetu na maisha yetu yawafikishie wengine ujumbe wa Mungu. Tukumbuke kwamba neno lake halirudi bure bila kuzaa matunda. Kulipokea ni baraka na fanaka kwa mwanadamu na kulipinga ni chanzo cha kuanguka na mauti.
SALA: Ee Mungu utujalie moyo wa usikivu ili tuweze kusikiliza vyema mafundisho yako. Amina.
Mungu ni mwema na anatulinda siku zote
KILA WAKATI MUNGU NI MWEMA.
Ok,nalishukuru shirika Kwa kuendelea kutupatia masomo ya Misa na tafakari zake.Mimi ni mtumiaji mkubwa wa ukurasa huu.Mungu AWABARIKI muendelee kutuhudumia.