Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika masomo ya Misa Takatifu 26/01/2024
2024 JANUARI 26 IJUMAA: JUMA LA 3 LA MWAKA
1/26/2024
Nyeupe
JUMA LA 3 LA MWAKA
Zab Juma 3
Wat. Timotheo na Tito, Maaskofu
Somo 1
2 Tim 1:1-8
Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa ajili ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu; kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Namshukuru Mungu nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana. Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha; nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo. Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu.
Wimbo wa Katikati
Zab 96:1-3, 7-10
Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. (K)
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.
Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)
Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika. (K)
Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)”
Injili. Mk 4:26-34
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara hupeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani? Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake. Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha.
TAFAKARI
UFALME WA MUNGU NI MEBGU NDOGO NDANI YETU: Katika Injili Yesu anafafanua namna ufalme wa Mungu unavyokuwa na kuenea. Kwanza ni kama mbegu inayopandwa. Mbegu hizi huota, hukua bila hata mwenye shamba kujua kinachofanyika. Wakati wa mavuno mwenye shamba huchukua mundu na kwenda kuvuna. Aidha, Yesu anaufananisha ufalme wa Mungu na mbegu ya haradali. Ni ndogo hivi, lakini ikishapandwa, ikishaota na kukua, huwa mmea mkubwa kuliko mimea mingi kiasi cha ndege kukaa kwenye matawi yake. Yesu anatumia mifano hii kutufundisha kwamba Mungu ndiye huusimika ufalme wake ndani yetu. Kama mbegu ufalme huo hauna budi kustawi na kukua. Kwa neema ya Mungu, ni jukumu letu sisi pia hatuna budi kuufanya ufalme huu ukue, uzae, uenee na uwafikie wengine. Tutambue kwamba tumebatizwa na tunatumwa kuustawisha ufalme huo wa Mungu. Tuombe basi neema ya kutambua wajibu wetu wa kuueneza ufalme wa Mungu.
SALA: Ee Mungu, utujalie kuwa udongo mzuri wa kustawisha mbegu ya ufalme wako ndani yetu. Amina.