Select Page

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 25/01/2024

2024 JANUARI 25 ALHAMISI: KUONGOKA KWA MT. PAULO, MTUME

Sikukuu

Kuongoka kwa Mt. Paulo, Mtume

Kuzaliwa: Tarso (Uturuki).

Utume: Alikuwa akiwakamata wakristu na kuwafunga minyororo. Alikuwa adui mbaya wa dini yaYesu.Baada ya kutokewa na Yesu njiani akielekea Dameski Sauli aliongoka na kusali na kufunga Sauli alibatizwa naAnania. Sauli akamhubiri Yesu kuwa ndiye Masiha.Akafanya kazi ya utume wa Kristo kwa moyo mkuu.

Nyeupe

Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1:  Mdo.  22:3-16

Paulo aliwaambia makutano, Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihada kwa Mungu kama nyinyi nyote  mlivyo leo hivi; Nikawaudhi watu wa Njia hii hata kuwauwa, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake. Kama kuhani mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote pia, ambao nalipokea barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili niwalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe. Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote. Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi. Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami. Nikasema, Nifanye nini, Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye. Na nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski.     Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na wayahudi wote waliokaa huko, akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile. Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia. Basi sasa, unakawilia nini? Simama, Ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.

WIMBO WA KATIKATI:                Zab.  117:1-2

Aleluya! Enyi mataifa yote, msifuni Bwana, Enyi watu wote, mhimidini.

(K) Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.

Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu, Na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)

INJILI:  Mk.  16:15-18

Yesu alionekana na wale kumi na mmoja, akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihuburi Injili kwa kila kiumbe.  Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.

TAFAKARI

TUMECHAGULIWA KUIENEZA HABARI NJEMA KWA WATU WOTE: Katika Sikukuu hii ya kuongoka kwa Mt. Paulo Mtume, tunashuhudiwa na Mtume Paulo mwenyewe, jinsi alivyoitwa na kuongoka. Mtume Paulo kabla ya kuongoka alikuwa akiwatesa Wakristo kutokana na kusimamia dini na sheria za kiyahudi, baadaye anapata maono na anatumwa na Kristo. Mtume Paulo anauliza jambo la kufanya na anaelekezwa. Anania anamweleza juu ya kuchaguliwa kwake na kwamba atamshuhudia Mungu kwa watu wote. Katika Injili tunamuona Yesu Kristo akiwatuma Mitume kumi na mmoja, wakaihubiri Habari Njema kwa kila kiumbe. Taifa la Mungu, kwa ubatizo wetu tunachaguliwa na tunafanywa Wakristo na kwa Sakramenti ya kipaimara tunapokea nguvu ya Roho Mtakatifu ili tuwe askari hodari wa Kristo na kumshuhudia. Kwa kuwa askari hodari tunadhihirisha ukakamavu wetu na uhodari wetu wa kushuhudia Habari Njema. Kwa mawazo, maneno na matendo yetu tunatangaza Habari Njema. Tunaalikwa daima kuyafanya mawazo, maneno na matendo yetu kuwa thabiti mbele Mungu na wenzetu.

SALA:Mungu Baba Mwenyezi, tunakukiri wewe kuwa ni ngao yetu na nuru yetu, tunakuomba Mwanga wa Roho Mtakatifu uendelee kuwa nasi ili tuweze kutangaza vema Habari Njema, amina