Select Page

Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa 22/01/2024

2024 JANUARI 22 JUMATATU: JUMA LA 3 LA MWAKA

Kijani

Zaburi: Juma 3

SOMO I:  2 Sam. 5:1-7, 10

Kabila zote za Israeli walimwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako. Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli watoke nje, na kuingia ndani. Naye Bwana akakuambia, Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli. Basi, wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni; naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za Bwana; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli.   Daudi alikuwa amepata miaka thelathili alipoanza kutawala, akatawala miaka arobaini. Huko Hebroni alitawala miaka saba na miezi sita; na katika Yerusalemu alitawala miaka thelathini na tatu juu ya Israeli wote na Yuda. Kisha mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu ili kupigana na Wayebusi, wenyeji wa nchi ile; hao ndio waliomwambia Daudi, wakisema, usipowaondoa vipofu, na viwete, hutaingia humu kamwe; huku wakidhania ya kuwa Daudi hawezi kuingia humo. Lakini Daudi aliipiga ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi.  Naye Daudi akazidi kuwa mkuu; kwa maana Bwana, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye.

WIMBO WA KATIKATI:              Zab. 89:19-21, 24-25

  1. Ndipo ulipowaambia watakatifu wako kwa njozi,

Ukisema:

Nimempa aliye hodari msaada,

Nimemtukuza aliyechaguliwa miongoni mwa watu.

(K) Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo. 

  • Nimemwona Daudi, mtumishi wangu,

Nimempaka mafuta yangu matakatifu.

Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake.

Na mkono wangu utamtia nguvu. (K)

  • Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo

Na kwa jina langu pembe yake itatukuka.

Nitaweka mkono wake juu ya bahari,

Na mkono wake wa kuume juu ya mito. (K)

INJILI:  Mk. 3:22-30

Waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo. Yesu akawaita akawaambia kwa mifano, Awezaje Shetani kumtoa Shetani? Na ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, ufalme huo hauwezi kusimama; na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake, nyumba hiyo haiwezi kusimama. Na kama Shetani ameondoka juu ya nafsi yake, akafitinika, hawezi kusimama, bali huwa na kikomo. Hawezi mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu, na kuviteka vitu vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu; ndipo atakapoiteka nyumba yake. Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele; kwa vile walivyosema, Ana pepo mchafu.


TAFAKARI

BWANA NI DIRA YA MAISHA YETU: Mapatano kati ya Wazee wote wa Israeli na Mfalme Daudi kule Hebroni yalifanyika mbele za Bwana. Baadaye wakamtia mafuta kuwa Mfalme wao. Waisraeli pamoja na Mfalme Daudi wanatambua kuwa Bwana ndiye dira yao, hivyo wanakubaliana mbele yake. Jambo hili limekuwa kinyume kwa Waandishi ambao waliamini kuwa Yesu anatoa pepo kwa Mkuu wa Pepo, ana Beelzebuli. Hawakuamini juu ya Nguvu ya kimungu aliyonayo, hivyo kukataa maongozi ya Mungu. Kitendo hiki kinaashiria kuwa hawakumtegemea Bwana kuwa dira yao. Na kitendo hicho kinachukua uzito wa kumkufuru Roho Mtakatifu. Wapendwa Taifa la Mungu, maisha yetu ni lazima yawe juu ya msingi wa imani juu ya Mungu. Mungu ndiye anayetuwezesha ndiye hasa dira yetu. Tukumbushwe na kauli inayosema, “Bwana ametoa na Bwana ametwaa”, Mungu ndiye anayetupa pumzi na ndiye anayeichukua, daima tumuelekee hasa kwa Sala.

SALA: Ee Bwana, tunatambua kuwa wewe ndiye mpaji wa yote, tunakuomba Neema ya kutambua kuwa wewe ni dira ya maisha yetu, daima utupe nguvu na ujasiri wa kukufuata daima, amina.