Tumsifu Yesu Kristu. Karibu katika masomo ya misa takatifu 21/01/2024
2024 JANUARI 21 JUMAPILI YA 3 YA MWAKA
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Yon 3: 1-5, 10
Neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili, kusema, Ondoka uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukaihubiri habari nitakayokuamuru. Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu, Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 25: 4-9
- Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha.
Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu.
(K)Ee Bwana unijulishe njia zako.
- Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako,
Maana zimekuwako tokea zamani.
Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako,
Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako. (K)
- Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)
SOMO 2: 1Kor. 7 : 29-31
Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana; na wale waliao kama hawalii; na wale wafurahio kama hawafurahi; na wale wanunuao, kama hawana kitu. Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita.
SHANGILIO: Mk. 1:15
Aleluya, aleluya,
Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia;
tubuni na kuiamini Injili.
Aleluya.
INJILI: Mk. 1:14-20
Hata baada ya Yohane kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri habari Njema ya Mungu, akisema, wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili. Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebadayo, na Yohane nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao. Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata.