Select Page

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masom ya Misa 20/01/2024

2024 JANUARI 20 JUMAMOSI: JUMA LA 2 LA MWAKA

Mt. Vinsenti, Shemasi na Shahidi

Kijani

Zaburi: Juma 2

SOMO I:        2 Sam. 1:1-4, 11-12, 17-19, 23-27

Ikawa baada ya kufa kwake Sauli, hapo Daudi aliporudi katika kuwaua Waamaleki, naye Daudi amekaa siku mbili katika Siklagi; hata siku ya tatu ikawa, tazama! Akaja mtu kutoka kambi ya Sauli, nguo zake zimeraruliwa, tena ana mavumbi kichwani mwake; basi, ikawa alipomfikia Daudi, akaanguka chini, akamsujudia.  akamwambia, umetoka wapi?Akamwambia, nimeokoka katika kambi ya Israeli. Daudi akamwambia, Yalikwendaje?Tafadhali uniambie. Akajibu, Watu wamekimbia vitani, tena watu wengi wameanguka wamekufa; hata Sauli naye na Yonathani, mwanawe, wamekufa.   Ndipo Daudi akashika nguo zake akazirarua; na kadhalika watu wote waliokuwa pamoja naye; wakaomboleza, wakalia, wakafunga hata jioni, kwa ajili ya Sauli na kwa ajili ya Yonathani mwanawe, na kwa ajili ya watu wa Bwana, na kwa ajili ya nyumba ya Israeli; kwa sababu wameanguka kwa upanga. Basi Daudi akamwomboleza Sauli, na Yonathani, mwanawe, maombolezo haya:  Wana wa Yuda na wafundishwe haya, walio fahari yako, Ee Israeli, juu ya mahali pako palipoinuka wameuawa; jinsi mashujaa walivyoanguka! Sauli na Yonathani walipendwa na kupendeza maishani wala mautini hawakutengwa; walikuwa wepesi kuliko tai, walikuwa hodari kuliko simba. Enyi binti za Israeli, mlilieni huyo Sauli, ambaye aliwavika mavazi mekundu kwa anasa, akazipamba nguo zenu dhahabu. Jinsi mashujaa walivyoanguka katikati ya vita! Ee Yonathani, wewe umeuawa juu ya mahali pako palipoinuka! Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, ulikuwa ukinipendeza sana; upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, kupita upendo wa wanawake. Jinsi mashujaa walivyoanguka, na silaha za vita zilivyoangamia!

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 80:1-2, 4-6

  1. Weweuchungaye Israeli, usikie,

Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi.

Wewe uketiye juu ya Makerubi, utoe nuru.

Mbele ya Efraimu, na Benyamini, na Manase,

Uziamshe, utuokoe.

(K) Ee Mungu, uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

  • Ee Bwana, Mungu wa majeshi,

Hata lini? Utayaghadhibisha maombi ya watu wako?

Umewalisha mkate wa machozi,

Umewanywesha machozi kwa kipimo kikuu.

Unatufanya sababu ya ugomvi kwa jirani zetu,

Na adui zetu wanacheka wao kwa wao. (K)  

INJILI:           Mk. 3: 20-21

Yesu aliingia nyumbani na mkutano wakakusanyika tena, hata wao wenyewe wasiweze hata kula mkate. Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili.

TAFAKARI

AKUFIKIRIAYE TOFAUTI NI YULE WA KARIBU YAKO: Yesu Kristo anaporejea nyumbani, jamaa zake walimtazama kama mtu aliyerukwa na akili. Tafsiri hiyo ni kutokana na matazamio yao ya awali kwa kuzingatia uwezo wa Kristo kwamba asingeweza kuyafanya. Walitegemea Yesu apate utajiri kutokana na kazi ya useremara, angewachukia viongozi wenye mamlaka katika kipindi chake kama vile walimu wa sheria, masadukayo, mafarisayo kutokana na namna walivyompokea, walitegemea asichangamane na makundi ya chini na wasiojiweza. Mambo yote haya yaliwafanya waone kuwa amerukwa na akili kwani haikutegemewa ajihusishe na mambo yaliyo kinyume na jamii yao. Hivyo wanamfikiria tofauti kutokana ukaribu wao wa kindugu naye. Sauli amekuwa akimfikiria tofauti Daudi hata akatamani kumuangamiza lakini fikra tofauti za Sauli zenye uovu zinabatilishwa na Daudi kwa fikra zenye upendo hasa baada ya kifo chake, kifo cha mwanae na waisraeli wengine. Ndugu zangu, katika maisha yetu kabla ya kufikiri tofauti tuwe na uhakika juu ya jambo tunalolifikiria. Jamaa za Yesu walitazama mambo yao katika mpango wa kibinadamu zaidi na si katika mpango wa Mungu.

SALA: Ee Mungu Mwenyezi tunakuomba utujalie Neema za kuongoza fikra zetu ili daima ziwe za upendo kwa wenzetu, pia tusiwe wepesi kufikiri vibaya juu ya wenzetu, amina.